Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

Serikali ya JK ilivyolainishwa na mabilioni ya Uingereza.

NA WAANDISHI WETU

Sakata la malipo tata ya dola milioni 6 (Sh. bilioni 12.7) kwenda kwa kampuni ya EGMA iliyokuwa ikiongozwa na kamishna wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na washirika wake limezidi kuibua mapya baada ya kubainika kuwa nguvu ya fedha hizo ilifanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuwahi kusimamisha kikao cha Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete.

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.
EGMA ni kampuni iliyopewa kazi ya kuwa mshauri katika mauzo ya hatifungani za dola milioni 600 (Sh. trilioni 1.3) ambazo Serikali ya Tanzania iliziuza kwa Benki ya Standard ya Uingereza, wamiliki wake wakiwa ni Kitilya, Gasper Njuu na aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Soko la Mitaji ya Umma Tanzania, Dk. Fratern Mboya, ambaye kwa sasa ni marehemu.

Maelezo ya kurasa 25 kuhusiana na mwenendo wa sakata hilo katika Mahakama ya London (Crown Court – Southwark), Uingereza, yaonyesha kuwa kazi ya fedha hizo ambazo ni asilimia 1 ya dola milioni 600 ya thamani ya hatifungani za serikali zilizonunuliwa na benki ya Standard ya Uingereza, ilikuwa ni kufanikisha biashara hiyo.

Kwenye ukurasa wa 30 wa taarifa hiyo, aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Uwekezaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Shose Sinare, ananukuliwa katika andiko lake la Mei 15, 2013, kwa ajili ya kuliwasilisha kwa Bodi ya Stanbic Tanzania, akieleza ni kwa namna gani EGMA ilivyowezesha kufanikiwa kwa mchakato wa mauzo ya hatifungani hizo.

Katika kipengele ‘e’ cha aya ya 158 ya maelezo hayo, Sinare ananukuliwa katika andiko lake akidai kuwa EGMA iliwasaidia katika kufanikisha mambo muhimu, akitaja mfano wa kwanza wa nguvu yake kuwa ni kuwahi kusimamisha kikao cha Baraza la Mawaziri cha Februari 27, 2013. (Haikufafanuliwa EGMA ilisimamisha vipi kikao hicho cha Baraza la Mawaziri).


Pili, Sinare ananukuliwa akisema kuwa EGMA iliwasaidia kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu (wakati huo Frederick Werema) kwa wakati, na pia kwa kushirikiana na Stanbic, wakafanikisha mazungumzo na Waziri wa Fedha wa wakati huo (Mei 2012), marehemu Dk. William Mgimwa. Kadhalika, Sinare ananukuliwa akisema kuwa mfano mwingine wa namna EGMA ilivyofanikisha manunuzi hayo kuwa ni kuwezesha nyaraka mbalimbali kufanyiwa kazi kwa wakati.

Aidha, Sinare ambaye anatajwa kuwa alijiuzulu Juni 3, 2013 kutokana na sakata hilo kama alivyofanya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Bashir Awale, anaeleza vilevile sababu za kutwaliwa kwa EGMA na kulipwa asilimia 1 ya mauzo ya hatifungani hizo kama ada ya ushauri kuwa ni pamoja na ukweli kuwa muamala huo ulikuwa wa kipekee, mkubwa sana na wa mafanikio, kuwapo kwa ushindani mkali wa zabuni, muamala ulipitia kamati mbalimbali za Serikali ya Tanzania na pia kupitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Tanzania.
“Jukumu lingine muhimu la EGMA… ni kufanikisha muamala kwa kufikisha nyaraka zinazotakiwa kutoka serikalini kwa wakati na kuwezesha mafanikio ya kukamilishwa kwa muamala,” inaeleza sehemu ya taarifa aliyonukuliwa Sinare katika andiko lake kwa bodi ya Benki ya Stanbic ya Tanzania.

SAKATA LENYEWE
Jumatatu wiki hii, Mahakama ya London, Uingereza ilibaini ufisadi wa Sh. trilioni 1.3 zilizotokana na mkopo uliotolewa na benki ya Standard ya Uingereza kwa serikali ya Tanzania.

Mahakama hiyo iliamuru serikali ya Tanzania irejeshewe Dola za Marekani milioni saba, baada ya kubainika kuwapo kwa udanganyifu huo. Baada ya kesi hiyo kufunguliwa kwenye mahakama hiyo na Taasisi ya Kupambana na Rushwa Kubwa Uingereza (SFO), ilibainika kwamba asilimia 1 ya mkopo huo ambayo ni Dola milioni sita zililipwa kwa EGMA ambayo inamilikiwa na Kitillya, ambaye kwa wakati huo alikuwa Kamishna Mkuu wa TRA.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alitoa taarifa ya Serikali Jumanne kuwa kuhusiana na sakata hilo na kusema kuwa baada ya uchunguzi kufanyika ilibainika kwamba Benki ya Uingereza iliitaka Tanzania ilipe mkopo huo na riba ya asilimia 1.4, lakini Stanbic Tanzania ilidanganya na kusema ulipwe asilimia 2.4 na asilimia moja ambayo ni nyongeza wakalipwa Egma.

NAMNA ILIVYOBAINIKA
Mwaka 2013 BoT iliikagua Benki ya Stanbic na kubaini kuwapo kwa malipo yasiyokuwa ya kawaida yaliyofanywa kwa kampuni ya Egma, ambayo yalikuwa kinyume cha taratibu za kibenki.

Fedha hizo, dola milioni 6, ziliingizwa kweye akaunti ya EGMA na ndani ya siku kumi fedha hizo zilitolewa na mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo, marehemu Dk. Mboya. Zilianza kutolewa kwa fedha taslimu Machi 18, 2013 (dola milioni 1.35; Machi 21, 2013 dola milioni 1.45; Machi 25, 2013 dola milioni 1.23; Machi 27, 2013 dola milioni 1.17 na kisha sehemu iliyobaki ya dola 590,000 ikahamishiwa katika akaunti ya kawaida ya EGMA kutoka kwenye akaunti maalum iliyokuwa ya kutwalia fedha hizo.

Baada ya BoT kufanya ukaguzi huo walitoa taarifa kwa serikali ya Uingereza kupitia SFO ambayo ilianzisha uchunguzi ambao ulisababisha kesi kufunguliwa.

Hata hivyo Benki ya Standard Group ambayo ni benki mama ya Stanbic Tanzania, imekiri makosa hayo na kukubali kulipa faini ya Dola milioni 25.2 (Sh. bilioni 54) kwa kosa hilo.

SEFUE, MASAJU WAFAFANUA
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema kwa sasa uchunguzi bado unaendelea kuhusiana na kashfa hiyo kwa wote waliohusika.

Alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inaendelea kuwachunguza watuhumiwa wote na uchunguzi ukikamilika taarifa itatolewa.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema pindi uchunguzi ukikamilika na wahusika wakibainika, taratibu za kuwafikisha mahakamani zitafuata.

CHANZO: NIPASHE
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top