Chambi Chachage
Tunajenga nyumba moja sasa
tunagombania fito za nini? Swali hilo litokanalo na msemo maarufu nchini
Tanzania linaweza kutumika kuelezea ukakasi uliojitokeza kuhusu Bajeti ya
Serikali. Wabunge machachari waliozuiwa kuendelea na vikao vya Bunge la Bajeti
wameamua kutafuta vilinge vingine. Huko nako wapo waliozuiwa.
Wadadisi wa mambo tunaamini ni
haki ya Kikatiba kwa mtu yeyote kujadili masuala yoyote yaliyo muhimu kwa
Taifa. Wasiwasi wetu ni kuwa ushabiki wetu wa kisiasa kuhusu sintofahamu
inayoendelea kati ya Serikali na baadhi ya wapinzani inaweza kutufanya tukose
utulivu wa kuchambua ni nini hasa wanachopingana kuhusu bajeti.
Hivyo basi, tumeamua kuchukua
fursa hii kuupitia ‘Uchambuzi
wa Bajeti Ya Serikali 2016/2017’ uliopangwa kutolewa kwa Umma na Kiongozi
wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, katika kongamano lao
lililozuiwa kufanyika Jumapili ya tarehe 12 Juni 2016. Lakini kwa kuwa
tunaamini kuwa mtazamo wa kiuchumi wa Waziri wa Fedha, Dakta Philip Mpango, una
ushawishi mkubwa kibajeti basi uhakiki wetu hauna budi kurejea na kulinganisha taarifa
nyingine muhimu za wizara yake.
Katika uhakiki wetu, uliojikita
kwenye sekta za kilimo na viwanda, hoja yetu kuu ni kwamba kuna ‘miingiliano
tata’ na ‘migongano hewa’ kati ya mipango ya maendeleo ya Serikali iliyotumika
kuandaa bajeti na makusudio ya uchambuzi wa wapinzani wanaojitanabahisha kama
wazalendo wanaofuata ‘Ujamaa
wa Kidemokrasia’.
Uchambuzi wa Kiongozi wa
wazalendo hao, kwa mfano, unakubaliana na Serikali kuhusu kujenga viwanda. Tena
unaipongeza “sana” bajeti yake ya sasa kwa kulenga “kuondoa changamoto ya miundombinu kwa kiwango
kikubwa sana.” Lakini unadai kwamba: “Miundombinu inaweza kujengwa lakini ikawa
haina watu wa kuitumia wala bidhaa za kusafirisha kwa sababu hakuna vivutio vya
kuanzisha viwanda pia.”
Pamoja
na kujaribu kuihuisha misingi ya Azimio la Arusha kuhusu sekta ya Umma kupitia Azimio
la Tabora, wazalendo hao hawatofautiani sana na Serikali kuhusu nafasi nyeti/tete ya sekta binafsi.
“Ikumbukwe kuwa Serikali haianzishi viwanda”, uchambuzi wao unasisitiza, “bali
inajenga mazingira mazuri ya wawekezaji kuanzisha viwanda.” Hivyo, unadai
kwamba bajeti hii ya Serikali “haijaweka hivyo vivutio vya kuanzisha viwanda na
imeminya uwezo wa walaji kutumia kwa kudhibiti matumizi na pia kutoza kodi
nyingi zinazopunguza uwezo wa kutumia bidhaa na huduma.”
Njozi
ya wazalendo hao ni kuona wananchi wengi wakiwa na ajira zenye tija. Ila
wanajua “viwanda vinachangia asilimia 20 ya ajira zote rasmi nchini na kwamba
theluthi mbili ya Watanzania wameajiriwa na sekta isiyo rasmi.” Hivyo, wanaona “juhudi
za kuongeza uzalishaji viwandani ni muhimu sana ili kuwaondoa Watanzania wengi
kutoka sekta isiyo rasmi na kuwaingiza kwenye sekta rasmi.” Ndiyo maana
kiitikadi hawaoni shida kuipima Serikali kwa “kutazama hatua mbalimbali za
kisera [za] kuwezesha sekta binafsi kufungua viwanda vingi zaidi nchini na kuajiri
watu wengi.’
Tathmini
yao inawafanya wadhani kwamba “Serikali ilipaswa kuja na Sera mahususi za
kufikisha asilimia 10 au zaidi ukuaji wa uzalishaji viwandani.” Ili kufanikisha
hilo wanadai “Serikali haina budi kukaa na wenye viwanda na kupata mwafaka wa
namna bora ya kuweka sera mahususi zitazopelekea uwekezaji mkubwa wa wenye
mitaji katika viwanda na kuongeza uzalishaji.” Yaani hawajaridhika na maneno
haya ya Dakta Mpango: “Bajeti hii imezingatia mawazo na mapendekezo ya wadau
mbali mbali wakiwemo wenye viwanda, wafanyabiashara na wengine wengi”? Wanataka
‘manahodha wa viwanda’ wawe na sauti zaidi? Mtazamo wa kiuchumi wa Kiongozi wao
usiopingana dhahiri na ‘dhana ya kibepari’ ya mapinduzi ya viwanda yatokanayo
na mapinduzi ya kilimo umepelekea uchambuzi wao pia udai kwamba:
“Kwa Uchumi wa Tanzania, ujenzi wa Sekta ya Viwanda hauwezi
kufanikiwa bila kukua kwa sekta ya kilimo. Kilimo ndio sekta Kiongozi katika
kutokomeza umasikini kwani inachangia theluthi moja ya Pato la Taifa na kuajiri
theluthi mbili ya Watanzania wote. Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya
Tano imeshindwa kufungamanisha Sekta ya Kilimo na ndoto ya maendeleo ya
Viwanda. Ushahidi wa kisayansi unaotokana na Taarifa za Serikali yenyewe
unaonyesha kuwa hakuna mahusiano kati ya mipango ya maendeleo ya viwanda na
mipango ya maendeleo ya wananchi. (Uk. 5).
‘Dongo’
hilo ni zito hasa ukizingatia kuwa katika Hotuba yake ya Kufungua Bunge ambapo
alimsifia Kiongozi huyo kwa ukomavu wa kisiasa, Rais alinena
haya:
“Sura ya
kwanza ya viwanda tunavyovikusudia ni vile ambavyo sehemu kubwa ya malighafi
yake itatoka ndani, hususan kweye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, na madini –
na maliasili nyingine. Viwanda vya aina hii vitatupa fursa ya kujenga mfumo wa
uzalishaji ndani ya nchi uliofungamana na kushikamana. Viwanda vya aina hii
vitahitaji na kutegemea malighafi toka kwa wazalishaji wa sekta nilizozitaja,
na kwa kufanya hivyo wazalishaji hao watakuwa na soko la uhakika humu humu
ndani ya nchi.”
Eneo mojawapo ambalo Bajeti kuu imejaribu kuzingatia alichosema Rais ni hili lilipo katika hotuba ya Dakta Mpango:
“Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye mafuta
ghafi ya kula (crude edible oil) yanayotambulika katika HS Code
1511.10.00 kwa mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuhamasisha kilimo
cha mbegu za mafuta hapa nchini na kukuza viwanda vya kutengeneza
mafuta ya kula. Aidha, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeandaa
mkakati maalum wa kuendeleza viwanda vya kuzalisha mafuta yanayotokana
na mbegu zinazozalishwa hapa nchini na kutumia fursa [ya] soko kubwa
lililopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania inayo nafasi
ya kuweza kuongeza uzalishaji wa mbegu za mafuta” (Uk. 87).
Mpango
wa Maendeleo Wa Miaka Mitano unapopelekea sasa kinachodaiwa kuwa ni asilimia
1 tu ya Bajeti ya Maendeleo iende kwenye kilimo, je, ni kwa sababu ‘vipanga’
waliouandaa hawaelewi muingiliano wake na viwanda? Je, ni kwa sababu huko serikalini
kuna ‘vilaza’ wa uchumi wa “viwanda vya kusindika mazao ya kilimo (agroprocessing industries)” ambavyo
uchambuzi wa wazalendo hao unavipigia chapuo?
Serikali
‘sikivu’ ya Rais Magufuli inajua fika inachotaka kukifanya kiuchumi hata kama
kuna dalili zinazoonesha kwamba haielewi kikamilifu inakoelekea na athari zake kwa undani.
Kama wadadisi tulivyowahi kugusia hapo awali kuhusu ‘Dakta
Mpango na Hatma ya Kifedha, Kibajeti na Kiuchumi’, njozi yake imejikita
katika ujenzi wa mkusanyiko wa viwanda vilivyojikita katika kile ambacho ‘wachumi
wa kiliberali’ wanakiona ni fursa ambazo uchumi wa nchi/jamii fulani unazo kuzidi
washindani wake.
Ukiirejea
taratibu ‘Taarifa
ya Hali ya Uchumi 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17’
aliyoiwasilisha Bungeni tarehe 8 Juni 216, kwa mfano, utakutana na mkakati wa “kuanzisha
kongane za viwanda (Industrial Clusters)
za kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo.” Hilo limejikita katika dhana ya
‘Minyororo ya kuongeza Thamani (Value
Chains)’. Na ndiyo maana hotuba yake ya ‘Makadirio
ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka 2016/17’
inasema:
“Serikali hadi sasa imeipatia Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania mtaji wa shilingi bilioni 60. Aidha, katika
hatua za awali, benki imeainisha minyororo 14 ya thamani ya mazao ya kilimo
katika sekta ndogo ndogo nane itakayopewa kipaumbele katika kutoa mikopo kwa
kuanzia. Sekta hizo ni za uzalishaji wa nafaka; mifugo; ufugaji wa samaki,
kilimo cha matunda, maua, mbogamboga, na viungo; mazao ya viwanda hasa miwa na
korosho; mbegu za uzalishaji mafuta ya kula; na mazao ya misitu hasa ufugaji wa
nyuki na mazao yake… kwa mwaka 2016/17, Benki imepanga kuendelea kutoa mikopo
kwa angalau minyororo 14 ya thamani (agricultural value chains) itakayofanyiwa
tathmini yakinifu kama iliyoanishwa kwenye mpango kazi wa kwanza wa 2016-2020”
(Uk 27 & 53).
Suala
la kilimo kwenye bajeti na mipango ya Serikali linazidi kutazamwa kwa jicho la
kibiashara/kiwekezaji. Ndiyo maana katika hotuba hiyo hiyo Dakta Mpango
anatujulisha kwamba madhumuni makuu “ya kuanzishwa benki hii ni kusaidia upatikanaji,
utoshelezi na usalama wa chakula endelevu nchini na kusaidia katika kuleta
mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha biashara ili
kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.” Picha hii inaakisi
maneno haya yaliyopo katika ‘Mpango
wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17’:
“Mradi [wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na Biashara] unalenga
kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini. Katika mwaka 2016/17 zimetengwa shilingi bilioni 1.227 fedha za
ndani kwa ajili ya: kuendelea kutafuta fursa nafuu za biashara na masoko kwa
bidhaa za kilimo na viwandani kupitia majadiliano baina ya nchi na nchi,
kikanda na kimataifa” (Uk. 92).
Usuli huo
unaweza kutusaidia kuelewa ni kwa nini Dakta Mpango alisema haya Bungeni: “Bajeti
hii pia inalenga kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuwekeza ili
kuvutia ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje katika kuendeleza viwanda na
kilimo.” Hakika mpango wa Serikali ya Magufuli siyo kujenga lile Taifa la
wakulima na wafanyakazi. Ni wa kujenga hili Taifa la wafanyabiashara na wawekezaji.
Viwanda
vilikuwa viwe vya wafanyakazi na kilimo kiwe cha wakulima enzi hizo za Ujamaa.
Ila enzi hizi za Uliberali viwanda vinatakiwa kuwa vya wawekezaji na kilimo kuwa
cha wafanyabiashara. Kama hatuamini hebu tutafakari haya maneno ya Dakta Mpango
wakati anawasilisha bajeti Bungeni: “Mheshimiwa Spika, azma kuu ya Serikali ni kuimarisha
sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa mtazamo wa kibiashara, kukuza viwanda na
kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na sekta hii.”
Dakta Mpango anaonekana amechoshwa sana na tija ndogo na kipato kidogo
katika kilimo. Sasa anatoa wito kwamba watu
watumie “nguvu” na “ubunifu” wao “katika kilimo cha mazao ya thamani kubwa.”
Ndiyo maana anataka “mapinduzi ya kilimo kutoka
kilimo cha kijungujiko (subsistence
farming) kwenda kilimo cha kibiashara.”
Je, mapinduzi hayo yanawezekana bila kuondoa idadi kubwa ya wakulima
kwenye ardhi/mashamba yao ili kuwapisha wenzao wachache wanaoonekana kuwa
wabunifu zaidi na wenye mtazamo wa kibiashara/kijasiriamali? Kama ni kweli
kilimo kinaajiri zaidi ya asilimia 70 nchini kama Dakta Mpango anavyodai, je,
lengo hasa la mipango na bajeti ya Serikali ni kuhakikisha watu wote hawa
wanabakia kwenye sekta hiyo?
Cha kushangaza ni kwamba swali hili la msingi katika stadi za
maendeleo ya uchumi haliguswi au
linapotezewa tu. Kwa mfano, Kiongozi wa ACT-Wazalendo anasema: “Kwa sisi
wachumi tunatambua kuwa ili kupunguza umasikini wa Tanzania kwa zaidi ya nusu
ilihitajika sekta ya Kilimo kukua kwa kati ya asilimia 8 na 10 kwa mwaka. Kwa
ukuaji huu tulionao sasa, maana yake itachukua miaka mingi sana watanzania
kuondoka kwenye dimbwi la umasikini. Baadhi ya mazao yanayotarajiwa kuzalisha
malighafi za viwanda uzalishaji wake umeporomoka kwa kiwango cha kutisha.”
Rai hiyo ya Wazalendo haiiambii Serikali inawezaje kukuza
sekta kwa ‘mwendokasi’ huo bila hata kuwa na mbadala kwa wakulima watakoachwa.
Inachoambulia kupewa ni mapendekezo yanayolenga “kumwezesha mkulima kubakia na
sehemu kubwa ya mapato yake na kuvutia wananchi wengi kujishughulisha na
uzalishaji katika kilimo.”
Ombi letu wadadisi ni kujibiwa hili tu: Tanzania ya viwanda ni Tanzania ya
kilimo?
CHANZO:UDADISI
Post a Comment