*Yamuomba radhi Okwi
Uongozi wa klabu ya Ruvu Shooting inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara umeomba radhi kufuatia tukio lisilo la kiungwana la mchezaji wake Mau Bofu kumpiga kiwiko mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi.
Bofu alifanya tukio hilo katika dakika ya 43 ya mchezo uliozikutanisha timu hizo Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Uhuru na kurushwa mbashara kupitia Azam Sports 2, na kusababisha Okwi asiweze kuendelea na mchezo na yeye kutolewa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema wao kama uongozi pamoja na mchezaji mwenyewe wamekiri kufanya kosa hilo na wanamuomba radhi Okwi mwenyewe, uongozi wa Simba pamoja na wapenda soka wote.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, uongozi wa Ruvu Shooting umefanya jitihada za kutafuta namba ya simu ya Okwi ili kuzungumza naye moja kwa moja lakini namba waliyopewa imekuwa haipatikani.
Bwire amekiri kuwa kitendo kile kiliigharimu timu lakini mchezaji mwenyewe ameomba msamaha na kusema hakudhamiria kufanya kitendo kile bali aliteleza kulingana na mazingira ya mchezo, jambo ambalo analijutia na kuahidi kutolifanya tena.
Post a Comment