Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

Utoro wa Wabunge wakwamisha Bajeti(Mwananchi)


Boniface Meena, Dodoma
UTORO wa wabunge katika vikao vya Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma jana ulikwamisha kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kupitishwa.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aliamua kuahirisha hatua za mwisho za upitishwaji bajeti hiyo baada ya kujiridhisha kuwa idadi ya wabunge waliokuwapo ukumbini wakati huo ilikuwa ndogo.
Kikatiba, wabunge waliopo ni 357 huku Bunge la sasa likiwa na wabunge wanaofikia 352, lakini hadi muda kikao hicho kilipoahirishwa jana, walikuwapo wabunge wasiozidi 110 tu.
“Sasa zoezi hili litafanyika Jumatatu (kesho) asubuhi kwa muda mfupi kisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto itasoma makadirio yake,” alisema Ndugai.
Naibu Spika aliahirisha kikao cha Bunge baada ya mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia kutoa hoja iliyokwamisha bajeti hiyo ambapo alitumia Kanuni ya Bunge inayoelekeza kuwapo kwa nusu au zaidi ya wabunge ili kupitisha bajeti.
Mbatia alitoa hoja hiyo baada ya kuhesabu idadi ya wabunge waliokuwamo ndani ya ukumbi huo wa Bunge, iliyobainika kuwa ni ndogo na hasa kwa wabunge wa CCM.
Hii ni mara ya kwanza kwa bajeti kushindwa kupitishwa kutokana na uchache wa wabunge waliohudhuria kikao cha bajeti.Katika kikao cha jana, baada ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza kujibu hoja na michango ya wabunge katika makadirio ya bajeti ya wizara hiyo, walisimama wabunge zaidi ya wanne wakiomba kutoa dukuduku zao.
Naibu Spika, Job Ndugai alitoa nafasi ya kwanza kwa Mbatia ambaye alitumia kifungu namba 112(1) cha masharti ya Kanuni ya 77 kinachosema kwamba, Kamati ya Bunge zima haitafanyika pale idadi ya wabunge waliohudhuria itakuwa bado haifikii nusu ya wabunge wote.
Baada ya kunukuu kanuni hiyo, Mbatia alisema amehesabu wabunge wote waliomo ukumbini na kubaini kuwa hawafiki nusu, hivyo bajeti haiwezi kupitishwa.“Naibu Spika nimehesabu zaidi ya mara mbili, wabunge hawafikii nusu inayotakiwa kwa ajili ya kupitisha bajeti.
Jumla ya wabunge wote ni 352 na waliopo hapa bungeni sasa hivi hawafiki 110 na nusu ya wabunge wote huwa ni 172 hivyo naomba kutoa hoja,” alisema Mbatia.
Baada ya Mbatia kuketi, alisimama Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali na kukazia hoja hiyo kwa kutumia Kanuni ya 77(1) na (2), inayohusu akidi za vikao vya Bunge naye alifuatiwa na Moses Machali wa Kasulu Mjini ambaye pia alikazia suala hilo.
Baada ya wabunge hao kuzungumza Naibu Spika alisimama na kueleza kuwa kanuni hiyo inaeleza pia kuwa hilo linaweza kufanyika kiti cha Spika kikiridhika au kutoridhia na kulichanganua.
Kufuatia kauli hiyo ya Ndugai, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisimama na kueleza kuwa haiwezekani suala hilo lisitolewe uamuzi wakati huo.
Ndugai alisimama na kujibu; “Lissu wewe na mimi nadhani tunapaswa kusaidiana kuongoza shughuli hapa kwa kuwa sisi ni viongozi, hivyo suala hilo nitalitolea uamuzi baadaye, tuendelee,” alisema Ndugai.
Wakati Bunge lilipoamua kukaa kama kamati na kuanza kupitisha vifungu vya wizara hiyo, wabunge wa NCCR, Mkosamali walikuwa wakizunguka ndani ya ukumbi wa Bunge jambo ambalo lilimfanya Naibu Spika kukemea.
“Wabunge Mkosamali na Machali najua mna kampeni mnayofanya, najua kila kitu kinachofanyika, hilo suala nitalifanyia uamuzi nikiridhika,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Hapa si shule ya msingi, muda wa kujifunza umeshapita, kuahirisha Bunge si kitu cha mchezo, hivyo naomba mtulie.”
Baada ya kusema hayo Bunge liliendelea kama kamati, huku baadhi ya wabunge wakionekana kurejea ukumbini kwa kasi ili kuongeza idadi, lakini hawakutosheleza.
Bunge liliporejea Ndugai alitoa uamuzi uliowiana na ombi la Mbatia kwa mujibu wa kanuni hiyo ya 77(3).
Alisema kanuni ya 77(3) inaposomwa inaeleza kuwa endapo Spika ataridhika kwamba idadi ya wabunge haikidhi akidi ataahirisha kupitishwa kwa bajeti.
“Kuna wabunge wako nje kwa idhini ya Spika, kuna wengine wako Zanzibar ambao ni 30 na kuna wengine wameniomba ruhusa wako kwenye msiba wa mama yake Mbunge wa Longido, Michael Lekule Laizer,” alisema Ndugai.
Alisema kuwa, ili kujiridhisha kwa kuhesabu anaondoa Kamati ya Bunge na zoezi la kupitisha vifungu hivyo vya Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika itamaliziwa Jumatatu baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Baadhi ya wabunge walilielezea tukio hilo kuwa ni la kihistoria ya tangu kuanzishwa kwa mfumo wa siasa wa vyama vingi nchini.
Makinda akerwaHivi karibuni Spika wa Bunge, Anne Makinda alieleza kukerwa na tabia ya utoro wa wabunge, ambapo aliikemea akiamuru kuwa mbunge yeyote, ambaye hatakuwapo bungeni anapaswa kuomba ruhusa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Makinda hakuishia hapo bali juzi alirejea onyo lake akisema kuwa baadhi ya wabunge wamekuwa na tabia ya kukacha vikao vya Bunge na kusafiri bila ruhusa.
Alisema kuwa kuna wabunge wanaosafiri bila kuomba ruhusa kwake wala kwa Waziri Mkuu na kwamba hali hiyo inaonyesha utovu wa nidhamu.
Kutokana na hali hiyo, Makinda alipiga marufuku wabunge kusafiri bila kupata ruhusa kutoka kwake au Waziri Mkuu.“Kuna wabunge wanatoka na kusafiri bila ruhusa, hivi mkipata ajali huko mtasemaje?,” alisema Makinda na kueleza kuwa tabia hiyo ikiachwa iendelee siku moja inaweza kusababisha kukwama kwa bajeti.
Katika hatua nyingine, wabunge wa NCCR walifanya kikao cha dharura jana kwa madai kwamba katika siku za nyuma Bunge lilipitisha mambo kadhaa kinyume cha utaratibu wa kuzingatia idadi ya wabunge waliomo ndani ya ukumbi.
Walisema kuwa kwa sababu hiyo watafanya uchunguzi wa kina ili kubaini mambo yaliyopitishwa katika mazingira hayo ili wapeleke hoja binafsi bungeni ili kuyatengua.
Hata hivyo, hawakutaja mlolongo wa mambo hayo waliyosema yalipitishwa na Bunge kinyume cha Kanuni za Bunge.
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top