KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Salum Msangi amemsweka rumande Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bariadi (OCD) na Mkuu wa Kituo cha Polisi Bariadi (OCS), kwa tuhuma za rushwa.Wakati hayo yakitokea, jeshi hilo limezidi kuandamwa na kashfa baada ya baadhi ya askari wake kudaiwa kumpiga Kadogoo Kalanga (16), hadi kulazwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Katika tukio la Simiyu, Kamanda Msangi anawashikilia maofisa hao kutokana na madai ya kuomba rushwa ya Sh3.5 milioni kutoka kwa mtuhumiwa kwa kisingizio RPC huyo ndiye aliyewatuma. Taarifa zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda Msangi, zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita saa 6:00 mchana, ambapo maofisa hao walimkamata mtu anayetuhumiwa kufanya ujambazi kwa kutumia silaha na kumtaka awape fedha hiyo ili wamwachie. Alisema maofisa hao wamechukuliwa hatua ili iwe fundisho kwa wengine ambao wanafanya kazi kwa mazoea na kulipaka matope jeshi hilo. Akisimulia tukio hilo, Kamanda Msangi alisema: “Maofisa hao wakiwa kazini waliarifiwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo… (jina tunalo) ambaye ni mfanyakazi wa Mgodi wa Barrick North Mara, akihusishwa na jambazi sugu aliyekuwa akitafutwa kwa kuhusika na tukio la uporaji dhahabu katika Mgodi wa Geita. “Mtu huyo alipokamatwa, ofisi yangu iliarifiwa na kuanza kufanya taratibu za kuwasiliana na watu wa Geita na maeneo mengine ili kubaini kama mhusika ndiye mtuhumiwa sahihi, ila kabla ya kukamilika kwa uchunguzi aliachiwa.” Alisema kitendo hicho kilimkera na kuamuru mtuhumiwa huyo atafutwe tena. Alisema baada ya kuwaagiza maofisa hao wamtafute mtuhumiwa, walipompata walimtaka awape kiasi hicho cha fedha na kumweleza kuwa wametumwa na RPC. Alisema ndugu wa mtuhumiwa huyo baada ya kuona wameombwa kiasi kikubwa cha fedha, walikwenda katika ofisi za RPC na kumweleza nia ya maofisa hao hali iliyomfanya aanze kuweka mitego ya kuwanasa. Alisema atahakikisha anasafisha idara zote za polisi mkoani humo hususan wenye tabia ya kuwabambikizia watu kesi. “Huo ndiyo msimamo wangu. Haiwezekani watu wafanye wanavyojisikia halafu tukae kimya wakati wanalipaka matope jeshi la polisi. Kabla ya kuwa mkoa, wilaya hii ilikuwa mbali na makao makuu ya Mkoa wa Shinyanga, hivyo watu walikuwa wakiishi kama kuku wa kienyeji,” alisema Msangi. Alisema yapo malalamiko mengi ya wananchi dhidi ya askari wa mkoa huo na kuahidi kuyashughulikia. Unyama Manyara Polisi mkoani Manyara, wanadaiwa kumpiga hadi kupoteza fahamu Kadogoo Kalanga, mkazi wa Orkesmet, wilayani Simanjiro juzi saa 5:30 asubuhi kwa madai kuwa ameiba mbuzi wa jirani yake. Kutokana na kipigo hicho, kijana huyo amelazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), katika Hospitali ya Selian, Arusha. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa alikiri kupata taarifa ya tukio hilo na kueleza kuwa tayari ameshatoa maelekezo kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Simanjiro kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha kwa ripoti. “Nimeshatoa maelekezo kwa OCD kwamba uchunguzi wa kina ufanyike na nipewe ripoti kamili kwa kuwa jana ndiyo nilipigiwa simu na kuelezwa juu ya tukio hilo,” alisema na kuongeza kuwa endapo kuna askari atakayebainika kuhusika na tukio hilo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo, mama wa kijana huyo, Paulina Kalanga alisema askari watatu walimfuata mtoto wake katika eneo la Mnadani na kumtuhumu kuiba mbuzi kisha kuanza kumpiga. Alisema walianza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kijana huyo kuanza kutokwa mkojo mfululizo kabla ya kupoteza fahamu. Huku akitokwa na machozi, mama huyo alisema askari hao wakati wakiendelea kumpiga, walimshika katika sehemu zake za siri na kuzivuta huku wakizigongagonga kwa kitako cha bunduki.“Walimkamata na kumpiga kwa marungu na mateke, hawakuridhika wakazishika sehemu zake za siri na kuanza kuzigongagonga na kitako cha bunduki. Nilimwona mwanangu akitokwa na mkojo na akapoteza fahamu.” Daktari: Hali mbaya Mkuu wa Kituo cha Afya cha Orkesmet, Dk Loishorwa Ole Yamak alikiri kumpokea kijana huyo kituoni hapo juzi na kueleza kuwa alifikishwa akiwa katika hali mbaya huku akitokwa na damu puani.“Ni kweli huyo kijana aliletwa hapa akiwa anatokwa damu puani kuna askari mmoja ndiye alimleta hapa na kutoa maelezo kwamba alianguka na pikipiki,” alieleza daktari huyo.Alisema baada ya kuona hali yake hairidhishi, aliwashauri ndugu wa kijana huyo wampeleke Arusha ili akapatiwe huduma ya CT-Scan na X-ray. Uchunguzi Morogoro Katika hatua nyingine, matokeo ya uchunguzi uliofanywa na madaktari mkoani Morogoro kubaini jeraha lililosababisha kifo cha mfuasi wa Chadema, Ally Zona wakati polisi wakitawanya maandamano ya chama hicho yametolewa na mwili huo umezikwa jana. Akieleza matokeo hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shillogile alidai kuwa jeraha lililosababisha kifo cha marehemu lililokuwa kichwani, lilitokana na kugongwa na kitu kizito kilichorushwa na siyo risasi kama ambavyo watu walikuwa wakidhani. Alisema uchunguzi huo ulifanywa na madaktari wawili wa mkoani hapa pamoja na Dk Ahmed Makata kutoka Dar es Salaam na kushuhudiwa na mwanasheria wa Chadema, Aman Mwaipaya pamoja na baadhi ya askari polisi. Alisema kuwa baada ya matokeo hayo ya daktari, polisi sasa wanaendelea na uchunguzi wa kubaini kitu hicho kilichorushwa na kusababisha kifo cha mfuasi huyo kabla ya kuchukua hatua za kisheria kwa askari au mtu mwingine atakayebainika kurusha kitu hicho ikiwa ni pamoja na kumkamata mtu au kiongozi wa chama hicho aliyechochea au kuandaa maandamano hayo yaliyozua vurugu. Serikali imeunda tume ya kuchunguza ikiwashirikisha polisi na watu wengine. Imeandikwa na Hamida Shariff, Morogoro; Moses Mashalla, Arusha na Frederick Katulanda, Bariadi. Chanzo:Mwananchi |
Loading...
RPC AMSWEKA RUMANDE OCD
Chediel . Powered by Blogger.
Post a Comment