*Ni ya kupinga filamu ya Wamarekani
*Shehe Ponda awatahadharisha polisi
WAISLAMU nchini, wanatarajia kuandamana wiki ijayo kupinga filamu iliyotengenezwa nchini Marekani na kumdhalilishaji Mtume Muhammad.
Hayo yamesemwa Dar es Salaam jana na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, alipokuwa akizungumza na MTANZANIA kwa simu.
Kutokana na hali hiyo, Shehe Ponda amelitaka Jeshi la Polisi nchini, kutojihusisha kwa namna yoyote na harakati za kuzuia maandamano hayo.
Sheikh ponda alisema kuwa, baada ya filamu hiyo ya Marekani kumdhalilisha Mtume Muhammad, waislamu hawawezi kukaa kimya na badala yake watalazimika kuandamana kupinga udhalilishaji huo.
“Maandamano hayo yatakuwa ni ya nchi nzima, lakini kwa sasa siwezi kusema yatafanyika siku gani kwa sababu tunafanya maandalizi ya kuyafanya wiki ijayo.
“Najua kwa kuyasema haya, kuna watu wengine watajitokeza kuyazuia, tunatoa wito kwao mapema waache kutuingilia katika mambo ambayo ni haki yetu na tuna uhuru wa kuyafanya.
“Jeshi la Polisi litambue wazi kwamba, sisi waislamu hatuna fujo, ni vema wakae pembeni kabisa waache tuandamane na kutoa tamko letu, vinginevyo ni kuanzisha machafuko.
“Leo nimewashangaa sana hawa polisi, wamefika mahali pa kulinda watu wanaofanya maovu, nimeshangazwa na kitendo cha kuweka ulinzi katika ofisi za makao makuu ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) na katika ofisi za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
“Tena katika ulinzi huo, polisi walikuwa na silaha, nashangaa sana, yaani mtu anayefanya makosa, badala ya kumkamata anaendelea kulindwa, hii haiwezekani,” alisema Shehe Ponda.
Alisema kwamba, filamu hiyo iliyotengenezwa na Wamarekani, inachochea uhasama na chuki baina ya wafuasi wa dini mbalimbali.
Kwa mujibu wa Shehe Ponda, filamu hiyo inadaiwa kutengenezwa na raia wa Israel mwenye uraia wa Marekani na kwamba imejenga mtazamo mbaya ndani ya jamii yote duniani.
Hata hivyo taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari zimemtaja mtengenezaji wa filamu hiyo ya Innocence of Muslims ni Sam Bacile, ambaye aliitayarisha kwa idhini ya Serikali ya Marekani.
Taarifa hizo zimeeleza kwamba, mtengenezaji huyo amejificha kusikojulikana, ambapo Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) na Vatcan, zimelaani filamu hiyo inayomvunjia heshima Mtume Muhammad.
Chanzo:Mtanzania
Loading...
Chediel . Powered by Blogger.
Post a Comment