Kwa ufupi
Stars itahitaji kupigana kiume kuishinda Sudan,
ambayo rekodi za viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Dunia
(Fifa) mwezi huu, vinaonyesha Sudan ikiwa nafasi ya 102 na Tanzania
nafasi ya 132.
TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) ikiwa 'full' kujiamini, leo inashusha karata yake ya kwanza ya michuano ya Chalenji dhidi ya Sudan ya Khartoum kwenye Uwanja wa Nambole, jijini Kampala.
Stars na Sudan ziko Kundi B, na mechi yao inatarajiwa kuanza saa 12 jioni, lakini awali ikitanguliwa na mechi kati ya Burundi na Somalia, saa tisa mchana.
Katika mtanange huo, Stars haitakuwa na kitu kingine cha kuhitaji zaidi ya kuibuka na ushindi ambao utaiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.
Stars itahitaji kupigana kiume kuishinda Sudan, ambayo rekodi za viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa) mwezi huu, vinaonyesha Sudan ikiwa nafasi ya 102 na Tanzania nafasi ya 132.
Kwa upande mwingine, kocha wa Stars, Kim Poulsen atakuwa na kazi ngumu ya kuhakikisha kikosi chake kinaibuka na ushindi ili kurudisha imani ya mashabiki.
Kabla ya kuondoka, Poulsen alisema anakwenda kuandika rekodi mpya akiwa na Stars yenye matumaini ya ushindi yaliyopitiliza.
Stars iliweka kambi jijini Mwanza badala ya Dar es Salaam kama ambavyo mara nyingi imekuwa ikifanya inapojiandaa na mashindano makubwa.
Poulsen anaamini kuwa mazingira ya hali ya hewa ya Mwanza yanaoana na yale ya Uganda kwa wakati huu, na hakuna shaka kikosi chake kimefurahia mazingira hayo.
Kikwazo kikubwa kwa Stars leo hii ni kukosekana kwa washambuliaji wake nyota, Mbwana Samata na Thomas Ulingwengu wanaocheza timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemkokrasi ya Congo.
Mazembe inayomilikiwa na tajiri, Moise Katumbi iligoma kuwaachia Samata na Ulingwengu kwa madai ya kwamba bado wana majukumu kwenye klabu yao.Kukosekana kwa nyota hao, kutamlazimu Poulsen kuwategemea Mrisho Ngasa na John Boko watakaosaidiana na Simon Msuva.
Safu ya ulinzi itaongozwa na Shomari Kapombe na Kelvin Yondan na hakuna shaka, Mwinyi Kazimoto na Frank Domayo kucheza nafasi ya kiungo.Kwa mara ya mwisho Stars ilitwaa ubingwa wa michuano ya Chalenji nje ya ardhi ya Tanzania mwaka 1994 ilipowachakaza wenyeji Kenya katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Nakivubo.
Chanzo:www.mwananchi.co.tz
Post a Comment