Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

SERIKALI 'YASALIMU AMRI' KWA ZITTO

  Yatamka kuzikubali hoja zake
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,
Sakata la ugunduzi wa uranium limezidi kuigawa jamii, huku serikali ikitamka dhahiri kuikubali hoja za Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.
Zitto alisema katika mjadala ulioendeshwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jana kuwa, kuzitegemea sheria na sera za gesi na mafuta, si njia sahihi ya kushughulia uzalishaji wa uranium nchini.
Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TDPC), Yona Killagane, kwamba Tanzania ina sheria na sera zinazosimamia sekta hiyo kwa ufanisi.
TPDC ni moja ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini inayoongozwa na Waziri Profesa Sospeter Muhongo.
Killagane alisema sheria na sera zilizopo zinaagiza kila hatua inayofikiwa katika utafiti wa gesi na mafuta, kupata kibali kinachohusu hifadhi ya mazingira kutoka kwa mamlaka husika.
Alizataka mamlaka hizo kuwa ni Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mkemia Mkuu wa Serikali na Wakala wa Afya na Usalama Kazini (Osha).
Alisema kabla ya kutolewa kibali hicho, mshauri mwelekezi anafanya tathmini ya athari zinazotokana na miradi ya mazingira.
Hivyo, Killagane alisema hakuna sababu kwa Watanzania kuwa na wasiwasi kwa vile kupitia sheria na sera zilizopo, serikali imejipanga ili pasitokee madhara kwa umma.
Mbali na Killagane, Mtaalamu wa afya ya mazingira (mafuta na gesi), alisema kutokana na sera na sheria zilizopo, hakuna athari za mazingira zitakazotokana na mradi wa uranium.
Lakini Zitto alipingana na hoja hiyo, akisema Tanzania ina sheria na sera nzuri ambazo hata hivyo hazisimamiwi inavyostahili. Alitoa mfano wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, kuwa pamoja na uzuri wake, jamii imeshuhudia kuwapo migogoro na matatizo kutokana na uwezo duni wa kuisimamia.
“Sidhani kama tumeandaa rasilimali watu wa kusimamia sera na sheria za gesi na mafuta,” alisema Zitto.
Kwa hali hiyo, Zitto alisema Tanzania imejisahau kuvijengea uwezo vyombo tofauti vinavyotumika kuisimamia sekta ya gesi na mafuta na kupendekeza kuwepo kitengo maalum cha kushughulikia maeneo hayo (gesi na mafuta).
Hali hiyo, ilimfanya Killagane kusema, “ninazikubali hoja za Zitto kuhusu kuwapo ukaguzi wa mara kwa mara, vyombo husika kujengewa uwezo na kuwepo kitengo maalum cha gesi na mafuta.”
Hata hivyo, Killgane, alisema serikali kupitia msaada wa serikali ya Norway, inatoa elimu kwa umma kwa masuala tofauti yanahusiana na gesi na mafuta.

AZUNGUMZIA GESI ASILIA TEMEKE
Ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, huenda ukaleta hasara badala ya tija iwapo gesi asilia yenye futi za ujazo zaidi ya trilioni 20 itagundulika wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam
Katika taarifa yake aliyoitoa kwenye mtandao wa Kijamii, Zitto alikariri taarifa za wataalamu kuwa huenda kuanzia mwakani, futi za ujazo wa trillioni 20 za gesi asilia zikapatikana kutoka kitalu namba 07 kilichopo Temeke.
“ Iwapo gesi nyingi itapatikana Dar es Salaam karibu na mitambo ya kuzalisha umeme, mradi huu wa bomba unaojengwa kwa trillioni za Shilingi utakuwa na maana, huo mkopo utakuwa na tija,” alihoji.
Bomba la gesi lenye kilometa zaidi ya 500 linajengwa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa mkopo wa Dola milioni 20.1 (takribani Shilingi bilioni 30) kutoka serikali ya China.
Alisema ingekuwa vyema kama serikali ingeangalia faida ya kujenga gridi nyingine badala ya kuwa na gridi moja inayotegemea bwawa la Mtera.
Zitto alisema kama bwawa la Mtera lisipozalisha umeme mitambo ya Dar es Salaam hata kama itazalisha megawati 10,000 hakutakuwa na umeme kwa kuwa uti wa mgongo wa gridi ya taifa ni bwawa la Mtera.
Alitaka kuwe na gridi nyingine itakayotumia gesi ya Lindi na Mtwara na kusisitiza kuwa ni lazima kuwasikiliza watu wa Mtwara

AUNGA MKONO MAANDAMANO YA MTWARA
Zitto alisema ni dalili za kushindwa kwa sera za serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuongeza.
“Kama hadi wananchi wa Mtwara ambako imekuwa ngombe ya CCM wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala ni dalili kuwa Watanzania wamefungua macho na wanaona,” alisema.
Alisema Mtwara wanataka viwanda na mitambo ya kusindika gesi na mbolea vijengwe mkoani humo kisha visafirishwe kwenda mikoa mingine.
“Hawasemi gesi na mazao yake vyote vibaki Mtwara na Lindi , wanachotaka ni umeme na mbolea vizalishwe Mtwara na kusambazwa sehemu nyingine, pia wanataka bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya Kusini,” alisema.
Aliwaunga mkono wananchi hao kuwa siyo dhambi kudai masuala hayo.
Alimkosoa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyewataka watu wa Mtwara kurudisha fedha za mkonge na kahawa.
“Mbona hajataja za korosho, mwaka jana korosho ilikuwa zao la pili kwa fedha za kigeni baada ya tumbaku,” alisema.
Alisema, wakazi wa Mtwara wamejifunza kutokana na yaliyotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita hivyo wanaandamana kuzuia yasiwakute.
“Mtwara wanahitaji kuungana na watu wa Mara, Mwanza, Shinyanga na Kagera kudai utajiri wa nchi utumike kwa maendeleo ya taifa badala ya kundi dogo la watu,” alisema. Aliwataka watu wa Mtwara kuunganisha nguvu na Watanzania wengine kuzuia uporaji wa rasilimali za nchi na kuwaonya wasijitenge kwani nguvu ya mnyonge ni umoja.
Wakazi wa Mtwara wiki hii waliandamana kusisitiza kuwa gesi iwanufaishe kwanza, badala ya kupelekwa Dar es Salaam nao wakiendelea kuwa maskini.  

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top