Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

KIVUMBI MAONI TUME YA KATIBA

Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu
*Wamiliki, wanahabari wataka uhuru wa habari utambuliwe
*Dk. Salim ahofia machafuko kutokana na mpasuko wa udini
TUME ya Mabadiliko ya Katiba jana iliendelea na utaratibu wake wa kukusanya maoni kutoka katika makundi maalum kwa kukutana na wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri na taasisi za kihabari.

Wakizungumza katika mkutano huo uliokuwa chini ya uenyekiti wa Profesa Mwesiga Baregu ambaye ni mjumbe wa tume hiyo, wawakilishi hao wa taasisi za habari wote kwa nyakati tofauti walitaka Katiba Mpya iwe na Ibara mahususi zinazotaja wazi wazi kuhusu kuwapo kwa haki na uhuru wa kujieleza, wa kupata habari, wa vyombo vya habari na uhariri.

Wa kwanza kuchangia katika mjadala huo alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari, Reginald Mengi ambaye alisema uhuru wa kutoa maoni uliobainishwa katika katiba ya sasa ni finyu na usiotoa kwa marefu na mapana uhuru na haki kwa vyombo vya habari kufanya kazi.

Akifafanua, Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kampuni za IPP alitaka kufutwa kwa sheria kandamizi kama Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 ambayo pamoja na mambo mengine inampa mamlaka waziri kulifungia gazeti pasipo kuhojiwa na yeyote.

Sambamba na hilo Mengi kama ilivyokuwa kwa makundi mengine ya habari yaliyotoa maoni yake jana, alitaka sheria inayotaka kusajiliwa kwa magazeti kwa kupata leseni kufutwa na hivyo kupanua wigo wa kidemokrasia wa kupata habari.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda ambaye ndiye aliyesoma utangulizi wa maoni ya wahariri alisema, wao katika mapendekezo yao kwa tume walitaka mabadiliko ya katiba mpya yaongeze vipengele vitakavyozingatia na kuhimiza kuhusu haki, uhuru, nafasi na wajibu wa vyombo vya habari katika taifa.

Kibanda aliwaeleza wajumbe wa tume hiyo kwamba, maoni ya jukwaa hilo ambayo yaliwasilishwa na mhariri mwandamizi, Deodatus Balile yalikuwa yanatokana na kazi waliyoifanya ya kupitia katiba za mataifa mbalimbali kama Marekani, Australia, Ghana, Kenya na Afrika Kusini.

Akiwasilisha maoni hayo rasmi ya jukwaa, Balile alisema wahariri walikuwa wakitaka kuwapo kwa ibara ambazo zilikuwa zikieleza bayana kuhusu haki na uhuru wa kujieleza, kupata habari na wa vyombo vya habari.

Mbali ya hayo, wahariri walitaka Bunge au mamlaka yoyote kutotunga kwa wakati wote sheria ambazo kwa namna moja au nyingine zitaingilia kwa njia yoyote uhuru na haki ya kutoa au kupata habari.

“Hakupaswi kuwepo vizuizi katika kuanzisha magazeti au vyombo vya habari binafsi, wahariri, wachapishaji wa magazeti na vyombo vingine vya habari hawapaswi kudhibitiwa au kuingiliwa na Serikali na au wasiadhibiwe au kusumbuliwa kutokana na mawazo au maoni wanayotoa kupitia tahariri au maudhui yaliyochapishwa na vyombo vyao.

“Vyombo vyote vya habari vya umma na binafsi vitoe fursa sawa na kuwezesha uwasilishwaji wa maoni na mawazo pinzani,” walisema wahariri.

Maoni yenye mwelekeo huo huo yaliwasilishwa pia na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari, Kajubi Mukajanga ambaye kwa upande wake alisema wao walikuwa wakisisitiza zaidi kuhusu uhuru wa uhariri.

Mbali ya hilo kama ilivyokuwa kwa jukwaa la wahariri, Kajubi alisema wao katika MCT walikuwa wakipendekeza kuundwa kwa Baraza Huru la Taifa la Habari ambalo lingetokana na wadau wenyewe.

Katika eneo hilo la Baraza la Habari, Jukwaa la Wahariri wao walitaka kuundwa kwake kuthibitishwe na Bunge na liwe likipata fedha kutoka katika Mfuko wa Hazina ya Taifa.

Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wajumbe wa tume hiyo, Dk. Salim Ahmed Salim aliwataka wanahabari na wamiliki wa vyombo vya habari

Kufanya kila wanaloweza ili kuliepusha taifa katika hatari ya kuingia katika machafuko ya udini kutokana na kile ambacho yeyé na wajumbe wenzake wa tume walikipata wakati wa kukusanya maoni yao katika maeneo mbalimbali nchini.

Dk. Salim alisema ametiwa hofu kubwa na kile alichokiona wakati wa ziara hiyo baada ya kubaini kuwapo kwa ufa mkubwa unaotokana na kukua kwa mbegu hatari ya udini.

Kutokana na hilo, Dk. Salim ambaye amepata kuwa Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Mataifa ya Afrika (OAU) alivitaka vyombo vya habari kutumia fursa walizonazo kuliepusha taifa katika zahama hiyo.

Akitoa mfano, Dk. Salim alisema katika taifa ambalo wananchi wake, wameoleana na wanaishi katika mikusanyiko ya Wakristo na Waislamu kuibuka kwa uhasama au machafuko yoyote katika misingi ya kidini yanaweza kulivuruga taifa kwa kiwango kikubwa.

“Lakini pia vyombo vya habari mtusaidie kukemea suala la udini ambalo limeanza kupamba moto katika nchi yetu. Ingawa utulivu na amani, vinategemea kuwepo kwa haki, lakini amani na utulivu haviwezi kufananishwa na kitu chochote, mtusaidie tusifike huko,” alisema Dk. Salim

Akizungumzia kuhusu hofu iliyoanza kujengeka kuhuru hatua ya tume hiyo kukusanya maoni ya makundi maalum pasipo kualika vyombo vya habari, Dk. Salim aliwahakikishia wananchi kutokuwa na wasiwasi, kwani hakuna maoni yoyote ya wananchi ambayo hayatazingatiwa.

“Wengine wanaweza kudhani labda maoni yao hayatazingatiwa. Tunawahakikishia hatutaficha chochote kitakachotolewa na wananchi. Tume hii inaundwa na watu wanaowakilisha makundi yote muhimu katika jamii. Hivi mnadhani inawezekana tukachakachua maoni ya Chadema wakati Profesa Baregu akiwamo humu!” alieleza Dk. Salim.

Katika hatua nyingine, wafugaji nchini wamekuja juu wakitaka Katiba mpya ijayo iwatambue kwamba nao ni wazalishaji na wachangiaji muhimu katika uchumi wa taifa.

Wanataka pia katiba hiyo, itamke wazi kwamba ardhi ni eneo pana la uchumi unaozingatia maslahi ya kila kundi, yaani wafugaji na wakulima.

Hayo ni baadhi ya maoni yaliyowasilishwa kwa tume ya kukusanya maoni ya Katiba na Adamu Ole Mwarabu, ambaye ni kiongozi wa jamii ya wafugaji wa kutoka Kilosa Morogoro.

Alisema kwa muda mrefu, wafugaji wamekuwa wakisukumwa nje ya mfumo wa kijamii kana kwamba wao si Watanzania na hawatambuliki kuwa mojwapo ya kundi muhimu la uzalishaji katika taifa.

Alisema, wafugaji kama kundi linaloingizia taifa pato kubwa lazima lipate uwakilishi maalum katika vyombo vya maamuzi kama bunge na katika halmashauri za wilaya.

Alisema, wabunge na wawakilishi wa sasa wanaotoka maeneo ya wafugaji wameshindwa kusimamia haki za wafugaji, ambapo kila mara wamekuwa wakisukumwa mbali pindi Serikali inapotaka kutenga maeneo ya hifadhi.

“Tunataka Katiba mpya, itambue ardhi jamii kama eneo pana la uchumi kwa kuzingatia maslahi ya kila kundi.

“Wafugaji tumekuwa watu wa kusukumwa tu kila siku, hatuna uhakika na mali zetu, tunaonekana kama wageni katika nchi yetu.

“Wafugaji tunayo mahitaji mengi, ikiwemo kuunganisha ufugaji na uchungaji katika mipaka ya nchi zilizopo kwenye Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

“Ni vema pia hizi sheria za Afrika Mashariki ziangaliwe upya ili zitambue matumizi ya ardhi ya wafugaji kuvuka mipaka ya nchi husika. “Kama wanyama wanatoka Serengeti na kwenda Masai mara kule Kenya bila kuzuiwa, kwa nini kizuizi hicho kiwekwe kwa mifugo yetu ambayo kimsingi wote ni wanyama?” alihoji Ole Mwarabu.

Aidha kiongozi huyo wa wafugaji, alitaka Katiba mpya iruhusu kuwepo kwa elimu za aina mbili katika maeneo ya wafugaji.

Alisema elimu hiyo ni ile ya kawaida ya darasani pamoja na ya asili inayotolewa na jamii yao ili kulinda utamaduni, mila, desturi na ustawi wa makabila yao.
 
CHANZO:MTANZANIA

author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top