Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

VIONGOZI WAKIRI KUFANYA KAZI KWA MAZOEA

VIONGOZI wa Serikali za vijiji, watendaji na wajumbe wa kamati mbalimbali za maendeleo, wamekiri kwamba walikuwa wanafanya kazi kwa mazoea, kwani hawakuwa na elimu ya utawala bora.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Pamoja Daima (PADA), Hamza Sung’he, wakati akitoa semina elekezi kwa viongozi wa vijiji vinne vya Wilaya ya Kisarawe.

PADA ilikuwa inamalizia kutoa semina kwa vijiji vya Kikwete, Mfuru, Chang’ombe na Masanganya baada ya vijiji vingine 12 kupewa semina hiyo mwishoni mwa mwaka jana.

“Tulikuwa tunafanya kazi kwa uzoefu, tulikuwa hatujui kitu lakini sasa baada ya kupata mafunzo ya utawala bora, tutafanya kazi kwa umakini na maendeleo yatapatikana,” alithibitisha Tatu Ibrahimu ambaye ni mjumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Kijiji cha Chang’ombe.

Sung’he alisema, lengo la mafunzo ni kupunguza urasimu ndani ya Serikali za vijiji na kuboresha huduma za maendeleo katika jamii, ili kuwa na ustawi na tija ifikapo mwishoni mwa mwaka 2015.

“Dhumuni la mafunzo ni kuongeza uelewa kwa wananchi na viongozi wao, kamati za maendeleo na kamati za uadilifu zitakazoundwa juu ya dhana nzima ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji kama msingi mkuu wa maendeleo.

“Kuboresha mahusiano kati ya viongozi wa Serikali za vijiji na wananchi, kuona kuwa viongozi wanajua majukumu yao na wanawajibika ipasavyo katika shughuli za kuleta maendeleo,” alisema Sung’he.

Alisema hadi sasa PADA imeweza kufikisha malengo yake ya kuvifikia vijiji vyote 16 vya Wilaya ya Kisarawe na kutoa mafunzo kwa viongozi ambao wakielewa maendeleo yatapatikana bila vikwazo.

Mafunzo hayo yalifanyika katika Shule ya Msingi Chang’ombe yenye walimu wanne wanaofundisha masomo yote kuanzia darasa la kwanza hadi la saba.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Willium Mjatta, alisema mafanikio mazuri kupatikana katika shule hiyo ni ndoto kwani idadi ya walimu haitoshelezi kutoa elimu bora kwa wanafunzi shule nzima.

“Tuko walimu wanne, wanafunzi 317, tunafundisha masomo yote lakini hatufuati ratiba za vipindi, hatuwezi kumaliza topiki kutokana na uchache wetu, hatuna muda wa kupumzika, tunatakiwa kwa kiwango cha chini tuwe walimu tisa.

“Tunafundisha kwa wasiwasi mkubwa kwa sababu madarasa mengine tunayotumia ni mabovu, taarifa za matatizo ya shule hii zipo kila ngazi lakini hatujapatiwa ufumbuzi wa matatizo yetu,” alisema.

Aliwaomba viongozi kujali matatizo yaliyopo katika shule za vijijini ili kuwapa moyo walimu wanaofundisha katika mazingira magumu.

CHANZO:MTANZANIA
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top