Nitafuatilia ahadi alizotoa Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe tarehe
17 Februari 2013 kuwa maji yataanza kutoka kata ya Goba tarehe 20
Februari 2013 na ziara ya Mkuu wa Wilaya Jordan Rugimbana kwenye kata
hiyo.
Hata hivyo, ni vizuri umma ukatambua kuwa pamoja na mabadiliko ya hoja
kwa kuongeza maneno ya kupendekeza hoja kuondolewa yaliyofanywa na
Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kinyume na kanuni za Bunge tarehe 4
Februari 2013, maelezo na hoja binafsi niliyowasilisha bungeni
yameongeza uwajibikaji wa Waziri wa Maji, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni na
Halmashauri kuhusu masuala ya maji.
Siku chache baada ya kutangaza tarehe 10 Februari 2013 kwenye mkutano wa
hadhara kuipa Serikali wiki mbili, Mkuu wa Wilaya na Meya wa
Halmashauri ya Kinondoni waliitisha mkutano na viongozi wa mitaa pamoja
na kamati za miradi ya maji ya jumuiya na leo tarehe 18 Februari 2013
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana ameanza ziara ya
ufuatiliaji wa miradi ya maji katika Jimbo la Ubungo.
Katika baadhi ya Halmashauri nchini ikiwemo za Jiji la Dar es salaam
yamekuwepo matumizi mabaya na udhaifu wa kiutendaji katika miradi ya
maji inayosimamiwa na Halmashauri kwa kushirikiana na kamati za maji au
jumuiya za watumia maji.
Itakumbukwa kwamba kwenye maelezo yangu ya hoja binafsi bungeni
nilieleza kwamba katika Halmashauri nyingi nchini ikiwemo za Jiji la Dar
es salaam yamekuwepo matumizi mabaya na udhaifu wa kiutendaji katika
miradi ya maji inayosimamiwa na Halmashauri kwa kushirikiana na kamati
za maji au jumuiya za watumia maji na nilitoa mifano ya Halmashauri ya
Kinondoni.
Katika maelezo yangu Bungeni nilitoa mfano wa Halmashauri ya Kinondoni
na kueleza kuhusu tatizo la maji katika kata ya Goba lililodumu sasa kwa
kipindi cha miaka zaidi ya mitano, pamoja na kwamba serikali
inaowajibu kulinda maslahi ya walaji na kuhamasisha upatikanaji wa
huduma ya maji kwa watumiaji wakiwemo wa kipato cha chini na walio
pembezoni au katika mazingira magumu mamlaka zinazohusika hazijaweza
kutimiza wajibu ipasavyo kuhusu kata ya Goba.
Jana tarehe 17 Februari 2013 Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe
kupitia mkutano wa hadhara wa CCM kama ambavyo imenukuliwa pia na baadhi
ya vyombo vya habari leo tarehe 18 Februari 2013 ametoa ahadi kwamba
kuanzia tarehe 20 Februari 2013 wakazi wa Goba wataanza kupata maji.
Kazi ya mbunge ni kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali, hivyo
nitaendelea kufuatilia ahadi hiyo ya Waziri ambayo ni sehemu ya ufumbuzi
wa muda mfupi kwa watu wachache lakini bado narudia kutaka majibu ya
Waziri wa Maji kuhusu ufumbuzi wa kudumu kwa Wizara kuchukua hatua za
ziada ili kata ya Goba itoke katika kupatiwa huduma ya maji chini ya
Manispaa ya Kinondoni na badala yake ihudumiwe na DAWASA pamoja na
DAWASCO ili kuwezesha uboreshaji mpana wa miundombinu.
Aidha, Waziri wa Maji, Mkuu wa Wilaya na Meya watoe majibu kuhusu
malalamiko ya wananchi ya kushindwa kushughulikiwa kwa matatizo ya
kimfumo kuhusu uendeshaji wa miradi ya maji, kutokutekelezwa kwa wakati
kwa vipaumbele vya maji kwa mujibu wa bajeti za Halmashauri
iliyopitishwa na madai ya ufisadi katika miradi inayosimamiwa na kamati
za maji au jumuiya za watumiaji katika baadhi ya maeneo kumesababisha
wananchi kukosa huduma ya maji.
Kwa mujibu wa maelezo niliyoyawasilisha kwa Serikali na kwa Bunge kwa
nyakati mbalimbali; historia ya tatizo hili inaonesha kuwa wakazi wa
Goba wameshawahi kuandika barua kwa Waziri wa Maji barua ya tarehe
15/10/2009 ikieleza kero ya maji kwa wananchi na wakimtaka alipatie
ufumbuzi tatizo hilo na nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa mkuu wa mkoa
wa Dar es salaam, na mkuu wa wilaya ya Kinondoni pamoja na hayo bado
tatizo linaendelea kutopatiwa ufumbuzi huku wakazi wa Goba wakiendelea
kukosa haki yao ya msingi kwa kuwa hakuna maisha bila maji.
Kushindwa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kulipelekea wananchi pia
kuandika barua ya wazi kwa waziri mkuu mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter
Pinda wakilalamikia mradi wa maji wa muda mrefu, pamoja na barua hiyo
hakuna jitihada kamili zilizofanyika za makusudi kuondoa tatizo hilo.
Utendaji mbovu na usimamizi mbovu wa miradi ya maji kwa manispaa ya
Kinondoni chini ya kamati za maji zilizosababisha maji kukatwa kwa
nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2007 na 2011 ndiyo chanzo cha ukosefu
wa maji kwa kipindi chote hicho.
Katika kipindi cha karibuni, kamati ya maji Goba baada ya kukatwa kwa
maji ilimwandikia barua mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni tarehe
30/08/2011 yenye kumbukumbu namba G/WP/GOBA/VOL013/11 ikimuarifu
Mkurugenzi kuhusu kusitishwa kwa huduma ya Maji kwa Wananchi wa Kata ya
Goba.
Katika barua hiyo ambayo mbunge nilipatiwa nakala yake, wananchi hao
walimlalamikia mkurugenzi kwa kutozifanya kazi barua zao wakionesha
mfano barua ya tarehe 22/05/2011 na kumuomba Mkurugenzi kuchukua hatua
za haraka ili huduma ya maji irejeshwe hata hivyo Manispaa ilizembea
kuchukua hatua zinazostahili.
Mnamo tarehe 21/03/2011, nilimwandikia barua Mkurugenzi wa Manispaa ya
Kinondoni yenye namba : KUMB:OMU/MJ/005/2011 yenye kichwa cha barua
“Hatua za Haraka zinahitajika kuhusu mradi wa Maji Goba” .
Kutokana na hatua stahili kutochukuliwa niliandika barua nyingine kwa
Mkurugenzi yenye kumb. OMU/MJ/008/2011 na kupendekeza hatua za haraka
kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha kutoka mfuko wa Jimbo
Tsh 3,000,000.00 zinapelekwa haraka katika Akaunti ya maji Goba ikiwa
ni sehemu ya kuchangia katika wajibu wa manispaa za kujenga uwezo wa
mradi husika na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni alifanya ziara Goba
tarehe 31/01/2012 katika ziara ile mkurugenzi aliwaahidi wakazi wa Goba
kurejesha huduma ya Maji ndani ya wiki moja lakini hadi sasa ni zaidi ya
mwaka wananchi bado hawajapata huduma hiyo.
Tarehe 18/03/2012 niliwaandikia barua tena DAWASA yenye kumbukumbu namba
OMU/MJ/006/2012 kuhusu hatua ambazo DAWASA imechukuakuhusu matatizo ya
maji katika kata ya Goba, katika barua hiyo nilitaka kujua hatua ambazo
DAWASA imechukua kushughulikia matatizo ya maji Goba hususani juu ya
kufanya majadiliano na Manispaa ya Kinondoni ili kuwa na mfumo endelevu
zaidi wa utoaji wa huduma ya maji katika kata ya Goba ambayo ina
ongezeko kubwa la wakazi, makazi na mahitaji mengine mengi kwa sasa.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
18/02/2013
Post a Comment