WANANCHI wa Mtwara wametoa masharti mazito wakiitaka serikali
iyatekeleze kwanza kabla ya kuanza kuchimba gesi asili na kuisafirisha
kwa njia ya bomba kwenda eneo Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza na Tanzania Daima mkoni humo hivi karibuni, baadhi ya
wananchi hao walisema kuwa sakata la gesi bado ni tete, na hivyo kuonya
kuwa serikali inapaswa kutafakari upya badala ya kutumia nguvu na
upotoshaji.
“Tunatambua gesi hii ni rasilimali ya Watanzania wote, lakini mikoa ya
kusini imesahaulika, na huu ndiyo msimamo wa wananchi wa mikoa hii bila
kujali itikadi za kisiasa. Gesi hii haitatoka bila serikali kuendeleza
mikoa yetu,” alisema mmoja wa wananchi hao.
Katika masharti hayo, wanataka kwanza serikali ikamilishe ujenzi wa
barabara ya Mtwara-Dar kwa kiwango cha lami, ujenzi ambao wanadai
umekuwa ukisuasua kwa miaka mingi, na hivyo kuleta shaka kama gesi
itaondoka bila miundombinu hiyo kukamilika, ni dhahiri watasahaulika
kabisa.
Pili, wanahitaji kujengewa uwanja wa ndege wa kisasa wenye kuruhusu
kutua ndege kubwa ili kuwavutia watalii na wawekezaji kuwekeza huko
pamoja na kupanuliwa kwa bandari ya Mtwara, jambo wanalodai litawapa
nafasi ya kusafirisha bidhaa zao kwenda kwenye masoko ya nje ya nchi
kirahisi.
“Unajua serikali ndiyo iliua viwanda vyetu vya korosho hapa Mtwara,
ikaleta wawekezaji kuchimba gesi Kilwa, halafu wakauacha mji huo hauna
umeme. Sasa tumeona ya Kilwa, hatuwezi kuacha gesi iende bila kuwekewa
viwanda, umeme wa uhakika na kufufua bandari yetu,” aliongeza mwananchi
mwingine.
Tanzania Daima ilibaini kuwepo pia kwa msigano mkubwa kati ya wananchi
na viongozi wa vyama vya kisiasa walioratibu na kuongoza maandamano ya
kupinga gesi kwenda Dar es Salaam yaliyofanyika Desemba 27, mwaka jana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema kuwa
wamewashtukia viongozi hao wa kisasa, kwani wamekuwa wanafiki na wenye
tamaa ya fedha baada ya kuketi na kulainishwa na serikali.
“Hatuwahitaji wanasiasa kwa sasa maana tumegundua wana ajenda zao za
kutaka kujinufaisha kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu 2015. Sisi kauli yetu
ni gesi kwanza, siasa baadaye. Wenzetu hawa walikwenda Dar es Salaam
wakakutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, na sasa wanazungumza lugha za
serikali. Hapa gesi haitoki,” alisema mmoja wa wananchi hao.
Tanzania Daima ilitaka kufahamu ikiwa hawaoni watachelewa kupata
maendeleo kutokana na msimamo wao huo, lakini majibu yao yalikuwa wazi
kwamba kama serikali haijajiandaa kuchimba rasilimali hiyo kwa ajili ya
watu wake basi iache, maana haiozi.
“Hayati Mwalimu Julius Nyerere kila mara alikuwa anasema kuwa aliacha
kuchimba madini kwa vile watu wetu hawakuwa wameandaliwa ili wanufaike.
Yalikaa miaka yote ardhini bila kuoza, hivyo hata gesi imekaa miaka yote
haijaoza kama hawawezi kutunufaishi waiache,” alisisitiza mwananchi
huyo.
Licha ya mikutano na maandamano ya kisiasa kuzuiliwa kwa muda na Jeshi
la Polisi mkoani Mtwara, Tanzania Daima limedokezwa kuwa wananchi hao
kwa sasa wanaendesha mikakati yao kupitia mikutano ya siri ambayo
inafanyika kwa ulinzi mkali.
Kwamba kwa siku wanafanya vikao visivyopungua vitano ili kupanga
mikakati ya kuhakikisha hawasalitiani na kuruhusu gesi hiyo kuondoka
bila matakwa yao kutekelezwa.
“Katika vikao vya karibuni tayari tumefikia uamuzi wa kuunda kikosi kazi
cha vijana, ambacho kimepewa jukumu la kuzunguka eneo zima la gesi ili
kuhakikisha hakuna bomba linalotandazwa na serikali kwa kushirikiana na
wawekezaji inaotaka wachimbe rasilimali hiyo,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment