Featured

  Featured Posts

  Social Icons

Loading...

TAARIFA KWA UMMA YAH: MAZUNGUMZO YA WABUNGE WA MKOA WA DAR ES SALAAM NA WAZIRI MKUU, DODOMA-TAREHE 07.02.2013

TAARIFA KWA UMMA
YAH: MAZUNGUMZO YA WABUNGE WA MKOA WA DAR ES SALAAM NA WAZIRI MKUU, DODOMA-TAREHE 07.02.2013
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda jana tarehe 7.2.2013 alifanya kikao na Wabunge wa Mkoa wa Dar Es Salaam na kuhudhuriwa na Waheshimiwa Abasi Zuberi Mtemvu ambaye ni Mwenyekiti wa Wabunge wa Dar es Salaam, Iddi Azzan, Mussa Azzan Zungu, Eugen Mwaiposa, Neema Himid, Mariam Kisangi, Phillipa Mturano, Halima Mdee, Dkt Milton Mahanga, Sophia Simba na Dkt Faustine Ndugulile. Kwa upande wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliwakilishwa na Waziri Anna Tibaijuka na Naibu wake Goodluck Ole Medeye. Kikao hiki pamoja na mambo mengine, kilijadili suala la Mji Mpya wa Kigamboni.
Katika kikao hiki  nilielezea kuwa dhana ya Mji Mpya wa Kigamboni ni nzuri, ila mchakato wa kufikia huko unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa sheria unaofanywa na viongozi na watendaji wa Wizara ya Ardhi. Nilitabanaisha kuwa sheria kama sheria ni nzuri na hazina matatizo yoyote, ila utekelezaji wa sheria hizi umekuwa na mapungufu makubwa.
Ikumbukwe kuwa mchakato huu unatawaliwa na sheria tano ikiwa ni pamoja na Sheria ya Utwaaji Ardhi na. 47 ya mwaka 1967; Sheria ya Mipango Miji na. 8 ya 2007; Sheria ya Ardhi no. 4 ya 1999; Sheria ya Wakala wa Serikali ya 1997 na Sheria ya Serikali ya Mitaa na.8 ya 1982.
Pili, ushirikishaji hafifu wa wananchi, viongozi wa Serikali na wawakilishi wa wananchi ikiwa ni pamoja na Mbunge wa eneo husika. Waziri na Watendaji wa Wizara wamekuwa hawafuati sheria na badala yake kumekuwa wakitumia ubabe, nguvu na usiri mkubwa katika utendaji kazi wao. Aidha, wananchi wamekuwa wakitaarifiwa na sio kushirikishwa katika mchakato wa mradi huu. Kuna tofauti kubwa kati ya kutaarifu na kushirikisha.
Aidha, kuongeza eneo la mradi toka ekari takribani 6,000 hadi kufikia ekari 50,000 bila kuwashirikisha wananchi wa maeneo ya Kisarawe II, Kimbiji, Pemba Mnazi na Somangila kumeleta taharuki kwa wananchi wengi wa maeneo haya.
Vile vile, uanzishaji wa Mamlaka ya kusimamia uendelezaji wa Kigamboni, Kigamboni Development Authority (KDA), umeleta mtafaruku mkubwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuhusu mamlaka na mipaka kati ya KDA na Manispaa, mamlaka ipi itenge bajeti ya kuendeshea kata chini ya Mradi huu na hatma ya Madiwani katika eneo la mradi.
Vile vile, kutokana na usiri mkubwa kwenye mradi huu wananchi wengi hawafahamu lengo la mradi, haki, stahili na hatma yao.
Katika kikao hiki nilitoa mapendekezo yafuatayo:
 1. Kufanya mapitio ya kisheria kuhusu taratibu na vifungu vya sheria vilivyokiukwa.
 2.  Kuandaa Mpango Kazi wa pamoja kwa kushirikiana na viongozi, wawakilishi wa wananchi pamoja Mbunge. Mipango yote iwe wazi kwa wananchi na kukubaliwa na wote.
 3. Viwango vya fidia viwekwe hadharani na kujadiliwa na wananchi na kuridhiwa.
 4. Ushiriki wa wananchi uwekwe wazi. Mtiririko wa manufaa kwa wananchi uwe kama ufuatao:
  1. Wananchi kuendeleza mwenyewe maeneo yao
  2. Wananchi kuingia ubia na wawekezaji katika maeneo yao
  3. Kuondoka eneo la Mradi kwa hiari baada ya kushindwa (4a-b).
 5. Wananchi watakaopisha eneo la mradi wapatie makazi mbadala. Serikali igharamie ujenzi wa makazi mbadala kwa ajili ya wakazi wenye kipato cha chini, kati na juu. Wananchi watakaohamishwa wapewe kipaumbele cha kwanza katika ununuzi wa makazi mbadala.
 6. Uhakiki wa wamiliki wa ardhi na nyumba ufanyike upya ili wale waliojenga baada ya zuio kuisha wapate fursa ya kuongezwa ikiwa ni pamoja maeneo mapya.
 7. Elimu ya kutosha itolewe kwa wananchi kabla ya mradi kuendelea.
 8. Majibu na makubaliano ya mapendekezo haya yawe kimaandishi.
HITIMISHO
Katika kuhitimisha. Waziri Mkuu alipitia mapendekezo na kusisitiza mambo yafuatayo:
 1. Masuala ya kisheria yaangaliwe kwa lengo la kuainisha mapungufu na maeneo yanayosigana kisheria hususan utendaji kazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke baada ya kuanzishwa kwa mamlaka ya KDA.
 2. Uwepo mfumo mzuri wa ushirikishaji wananchi kuanzia ngazi za mitaa, na kutengeneza mfumo wa mawasiliano na uwakilishi. Aidha aliongeza kuwa ni vyema pia wanaharakati wakawa kwenye kamati hizi. Vile vile kwa kuwa mradi huu ni mkubwa, ni vyema Wabunge wa Dar Es Saalaam hususan wale wa Kigamboni wakashirikishwa kikamilifu katika mchakato mzima na kuwepo mikutano ya mara kwa mara ya mrejesho. Ajenda hii iwe ya kudumu na elimu ya kutosha itolewe kwa wadau wote.
 3. Wizara iainishe namna gani wananchi watafaidika na mradi huu. Aliagiza mapendekezo niliyotoa kuhusu manufaa kwa wanachi yafanyiwe kazi.
 4. Alishauri zoezi la uhakiki na tathmini lifanyike upya.
 5. Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa makazi mbadala kwa wale watakaohamishwa kuwa katika  maeneo ya karibu na Kigamboni.
 6. Aliwataka Mawaziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kufanyia kazi maagizo haya pamoja na changamoto zilizoainishwa na maelezo au ufafanuzi kuletwa katika kikao kingine kitakachofanyika Dar Es Salaam katika siku za karibuni.
 7. Mwisho, Waziri Mkuu alisisitiza matumizi ya lugha ya staha pamoja na kujenga “Partnership Dialogue” ili mradi uweze kwenda vizuri.
Napenda kuwashukuru Wabunge wa Mkoa wa Dar Es Salaam kwa ushirikiano walioonyesha na kwa michango mizuri katika kikao hiki. Kwa aina ya pekee, ninamshukuru Waziri Mkuu, kwa kuendesha vizuri kikao hiki kwa hekima na busara.
Ninawaomba wananchi wa Kigamboni kuendelea kuwa watulivu, wakati mimi na Wabunge wenzangu wa Dar Es Salaam tukiendelea kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu na pia majibu ya hoja zilizotolewa. Mwisho, niwatake Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuendesha mchakato huu kwa mujibu wa sheria, kwa kuzingatia dhana ya utawala bora na kwa taratibu shirikishi.
Dkt Faustine Ndugulile (MB)
JIMBO LA KIGAMBONI
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top