*Wakutana mjini Iringa kuijadili Serikali
WANAFUNZI waliofeli mtihani wa taifa wa kidato cha nne, wamekutana mjini Iringa. Wanafunzi hao walikutana jana saa tano asubuhi, katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtakatifu Augustino cha Ruaha (RUCO) kwa uratibu wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu.
WANAFUNZI waliofeli mtihani wa taifa wa kidato cha nne, wamekutana mjini Iringa. Wanafunzi hao walikutana jana saa tano asubuhi, katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtakatifu Augustino cha Ruaha (RUCO) kwa uratibu wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu.
Katika mkutano huo, wanafunzi zaidi ya 400 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa, walijaa ukumbini na wengine walilazimika kusimama nje ya ukumbi kwa kuwa ukumbini hakukuwa na nafasi.
Baada ya mjadala kuanza, baadhi ya washiriki waliokuwa wakipewa nafasi ya kuzungumza, walikuwa wakishindwa kujieleza, badala yake walikuwa wakilia kuonyesha ni kwa jinsi gani wasivyoridhishwa na matokeo yao.
Wengine badala ya kuonyesha masikitiko yao, walikuwa wakiishutumu Serikali wazi wazi kwa kile walichokuwa wakisema kwamba wamefeli kutokana na uzembe uliofanywa na waliosahihisha mitihani yao.
Hata hivyo, wakizungumza katika kikao hicho, wanafunzi hao walisema licha ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuunda tume ya kuchunguza matokeo hayo, ikubali kulegeza masharti ya kujiunga na vyuo vya ufundi na vyuo vinginevyo ili waweze kupata elimu wanayoihitaji.
Mmoja wa wanafunzi hao, Gerald Kiyeyeu, aliyehitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya St. Michael, alisema kwa kuwa baadhi yao wanaamini wamefelishwa, kuna haja kwa Serikali kuruhusu mitihani hiyo isahihishwe upya ili ukweli halisi upatikane.
Kwa mujibu wa Kiyeyeu, kama matokeo hayo yataachwa kama yalivyo, wanafunzi wengi wataharibikiwa maisha, wakiwamo wanaotoka katika familia masikini.
”Tunakuomba Mwenyekiti uzungumze na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi (Dk. Shukuru Kawambwa) ili mitihani yetu isahihishwe upya na wale wanaotaka kurudia mitihani yao wagharamiwe na Serikali, kwa vile vituo vinavyotoa huduma hiyo vinatoza gharama kubwa kuliko uwezo wetu,” alisema Upendo.
Naye Upendo Vitus aliyehitimu katika Shule ya Sekondari Tagamenda, alimwambia Mwenyekiti huyo wa CCM, kwamba wanachotaka wao Serikali iruhusu mitihani isahihishwe upya ili ukweli ujulikane.
Alisema kwamba haoni umuhimu wa tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kuwa haitakuja na majibu yanayoaminika.
Kutokana na hali hiyo, alisema kinachotakiwa ni Serikali kukubali mitihani hiyo isahihishwe upya, ikiwa ni pamoja na kugharamia masomo kwa watakaotaka kurudia kidato cha nne mwaka huu.
Naye Msambatavangu alipokuwa akizungumza katika mkutano huo, aliwataka wanafunzi hao kutoyumbishwa na kauli za wanasiasa, kwa kuwa wanasiasa wanaweza kuwatumia vibaya kupitia matokeo mabaya ya kidato cha nne.
Pia, aliwataka baadhi yao waliokuwa na mawazo ya kujiua, wasifanye hivyo japokuwa wazazi wao wanawasema vibaya baada ya kufeli mtihani huo.
”Hakika hamtajuta kwa uamuzi huu niliouchukua wa kukutana na nyie kwa sababu nimeumia sana moyoni mwangu na nikalazimika kusema lazima kuna kitu kifanyike kwa ajili yenu.
”Nimeshafanya mazungumzo na baadhi ya vyuo vikuu vya hapa kama Tumaini na RUCO ili waangalie namna ya kuwasaidia kwa kuandaa kozi za muda mfupi hadi mwezi Mei mwaka huu.
”Lengo la kuandaa kozi hizi ni kuwanoa ili baadaye tuone kama wapo wanaoweza kusaidiwa kwa kuendelea na elimu ya ngazi ya cheti.
”Najua kuna wanasiasa pamoja na wanaharakati watajiingiza katika hili, lakini tambueni kwamba, huu siyo wakati wa wanasiasa, wanaharakati na wadau wa elimu nchini kupigana mawe kutokana na anguko hili.
”Ila kinachotakiwa hapa ni Serikali ya CCM na watendaji wake, kujipanga upya na kutazama ni kwa namna gani kundi la wanafunzi waliofanya vibaya katika mitihani yao wanaweza kusaidiwa.
”Nayasema haya kwa sababu inawezekana mliopata sifuri na kuonekana hamna maana, mkawa kioo katika maisha na waliowacheka na kuwabeza, wakawaheshimu kutokana na mchango wenu katika elimu hapo baadaye.
”Nawaomba sana msikate tamaa, maisha ni safari ndefu kwa sababu kufeli mitihani si kufeli maisha, unaweza ukafeli mtihani lakini kwa kuwa Mungu ana mipango yake kwa kila mtu, unaweza kuwa mtu wa maana kuliko hata yule aliyefaulu,” alisema Msambatavangu.
Naye Mkurugenzi wa Kozi Fupi na Masomo Endelevu katika Chuo cha RUCO, Baby Chuma, aliwataka wanafunzi hao kutokata tamaa kwa kuwa kufeli kidato cha nne siyo kufeli maisha.
Aliwataka pia wajiendeleze kwa kujiunga na kozi mbalimbali za masomo ili baada ya miaka miwili, wawe na sifa ya kujiunga na vyuo vikuu.
Katika utekelezaji wa suala hilo, alisema menejimenti ya RUCO, imeshakubaliana na kiongozi huyo wa CCM ili kozi fupi zitolewe kwa waliofeli mitihani hadi Mei mwaka huu.
Kwa upande wake, Msajili wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini (IUCo), Melckzedeck Nduye, aliwahakikishia wanafunzi hao, kwamba chuo hicho kimeungana na wadau wengine kutoa huduma kwa wanafunzi waliofeli kuanzia Machi, mwaka huu.
Wakati hao wakisema hayo, Mratibu wa Uhamasishaji wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), Wilaya ya Iringa, Aidan Salehe, alipoulizwa kuhusu matokeo hayo ya kidato cha nne, alisema baraza hilo limepanga kuwaunganisha wanafunzi hao kwa kuitisha maandamano ya kulaani matokeo hayo.
”Maandamano yako pale pale, mazingira mabovu ya elimu, mitaala mibovu na uongozi wa aina hii, ndio tunataka vijana wausemee wenyewe.
”Katika hili alichokifanya Mwenyekiti wa CCM ni kizuri kabisa na kinapaswa kupongezwa, lakini ukweli ni kwamba, ameamua kuwakutanisha waliofeli kwa sababu anajua tukiandamana tunaweza kuchota wanachama wengi zaidi wakiwamo wa CCM,” alisema Aidan.
Katika matokeo hayo ya kidato cha nne yaliyotangazwa wiki iliyopita, Mikoa ya Iringa na Njombe ilikuwa na wahitimu 15,428, lakini asilimia 89 walipata alama sifuri.
Wakati akitangaza matokeo hayo, Dk. Kawambwa alisema watahiniwa 480,036 walisajiliwa nchini kote kufanya mtihani lakini waliofanya mtihani ni 397,136. Pia alisema jumla ya watahiniwa 126, 847 kati ya 397,136 waliofanya mtihani huo wamefaulu huku watahiniwa 270,289 hawakufaulu.
Katika matokeo hayo, alisema waliopata daraja la kwanza ni 1,641, daraja la pili ni 6,453, daraja la tatu ni 15,426, na darala la nne ni 103,327
NA MTANZANIA.
Post a Comment