Kamishsina wa Polisi Musa Ali Musa akitoa ufafanuzi
...............
UJIO wa Askari wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) nchini
na kuanza kufanya kazi, umewezesha kuanza kunaswa kwa baadhi ya watu,
wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya Padre Evarist Mushi (55) wa Kanisa
Katoliki Unguja, visiwani Zanzibar.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi
Jumamosi Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa
alithibitisha kwamba jeshi lake limekuwa likishirikiana na FBI katika
upelelezi huo na kwamba idadi ya waliokamatwa imeongezeka.
“Ni kweli tumekuwa tukishirikiana na FBI katika
upelelezi ili kuhakikisha kuwa, wahusika wa tukio la kuuawa kwa Padri
Mushi wanakamatwa. Hii itasaidia kupunguza vitendo vinavyohusishwa na
matukio ya kigaidi yakiwamo mauaji,”alisema Kamishna Musa.
Alisema kuwa hilo linafanyika ili kuhakikisha
kuwa, zoezi la kuwakamata wahusika wa uhalifu huo linafanikiwa kwa kiasi
kikubwa, jambo alilosema linaweza kupunguza matukio ya mauaji.
Alibainisha kwamba hadi sasa kuna ongezeko la
idadi ya watu waliokamatwa na kwamba watu hao wanaendelea kuhojiwa, huku
wengine wakishikiliwa kwa sababu maalumu.
Kamishna Musa alifafanua kuwa kutokana na zoezi
hilo watu watakaobainika kuhusika na mauaji hayo watafikishwa kwenye
vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua zaidi.
Padri Evaristus Mushi aliuawa Februari 17, mwaka
huu kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana waliokuwa katika pikipiki
aina ya Vespa, wakati akienda kuongoza misa katika Kanisa la Mtakatifu
Theresia la Beit el Rass.
Juzi, Kamishna Musa aliliambia Gazeti hili kwa
njia ya simu kwamba wapelelezi wa kigeni wamewasili Zanzibar kufanya
uchunguzi wa kuwabaini waliomuua kwa kumpiga risasi, Padri Evarist
Mushi.
Alisema kuwa wapelelezi hao tayari wameanza kazi
hiyo kushirikiana na wenzao wa Tanzania kuwasaka wauaji wa padri huyo
aliyepigwa risasi Februari 17, mwaka huu.
“Wapelelezi kutoka nje wamefika na wapo kazini,” alisema Kamishna Mussa bila ya kutaja wanatoka nchi gani.
“Wapelelezi kutoka nje wamefika na wapo kazini,” alisema Kamishna Mussa bila ya kutaja wanatoka nchi gani.
Pia Kamishna Mussa hakutaka kueleza ni lini
wapelelezi hao walifika Zanzibar na idadi yao kwa maelezo kwamba hizo ni
siri za polisi na kwamba zikivuja, zitaingilia uchunguzi
wanaoufanya.
Hata hivyo, vyanzo vya ndani ya Serikali, vililithibitishia
Mwananchi kuwa FBI walikuwa wameanza kuwasaka wauaji wa Padri Mushi.
Kutua kwa wapelelezi hao wa Marekani kunafuatia
kauli iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete katika salamu zake za
rambirambi baada ya mauaji ya Padri Mushi, kuwa amewaagiza polisi
kutumia nguvu zake zote pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya
usalama vya ndani na mashirika ya upelelezi ya nchi rafiki katika
kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.
Awali, akitoa tamko la Serikali na kueleza kuwa
Rais Kikwete ameidhinisha Serikali kugharamia wapelelezi kutoka nje,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alihusisha tukio
hilo na vitendo vya ugaidi.
Ujio huo wa FBI pia unaweza kuhusishwa moja kwa moja na dhamira
iliyoonyeshwa mapema na Serikali ya Marekani kuwa ipo tayari kusaidia
upelelezi wa mauaji hayo.
Dhamira hiyo ilibainishwa katika salamu za
rambirambi za kifo hicho zilizotolewa na Balozi wa Marekani nchini,
Alfonso Lenhardt.
Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya Serikali vimeeleza
kuwa kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo, maofisa wa FBI walifanya
mazungumzo na Waziri Nchimbi na viongozi wengine wa Serikali kwa ajili
ya kuangalia namna watakavyofanya shughuli hiyo.
NA MWANANCHI.
NA MWANANCHI.
Post a Comment