WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda
..............
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, ametangaza kikosi kazi kinachounda
tume itakayochunguza chanzo cha kufeli kwa asilimia 60.5 ya
watahahiniwa wa Mtihani wa Kidato cha IV mwaka jana nchini.
Tume hiyo inayoundwa na watu mbalimbali wakiwamo
wabunge, wasomi, viongozi kutoka taasisi za kidini na wadau wa elimu,
ilitangazwa jana jijini Dar es Salaam na itaongozwa na Katibu Mtendaji
wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini, Profesa Sifuni Mchome.
Waziri Mkuu Pinda aliwataja wajumbe wengine wa
tume hiyo kuwa ni pamoja na James Mbatia Mbunge wa kuteuliwa, Bernadetha
Mshashu Mbunge wa Viti Maalumu na Abdul Marombwa Mbunge wa Kibiti.
Wengine ni Profesa Mwajabu Possi kutoka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Honorath Chitanga Makamu wa Rais Chama cha Walimu
Tanzania(CWT), Daina Matemu Katibu, Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa
Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA).
Wajumbe wengine ni Rakhesh Rajan, Katibu Mtendaji wa Shirika lisilokuwa na Kiserikali (NGO) Twaweza.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo
Binafsi nchini (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo na Mratibu wa Taasisi ya
Kukuza Mitalaa, Kizito Lawa.
Wengine ambao watatoka katika taasisi za dini ni
Peter Maduke ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Kikristo la
Huduma za Kijamii (CSSC), Nurdin Mohamed Mkuu wa Chuo cha Ualimu
Alharamain iliyopo chini ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Wajumbe wa kutoka Zanzibar ni Suleiman Hemed
Khamis mjumbe kutoka Baraza la Wawakilishi, Abdalla Hemed Moh’d wa Chuo
Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA ) na Mabrouk Jabu Makame wa Baraza la
Elimu Zanzibar.
Akitangaza kuundwa kwa tume hiyo Pinda alisema
matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012, yameonyesha kuwa
kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa kiasi kikubwa, ikilinganishwa na mwaka
2011.
Matokeo hayo yameonyesha kuwa kati ya wanafunzi 397,132 waliofanya mtihani huo, watahiniwa 126,851 ndiyo waliofaulu.
“Katika idadi hii ya wanafunzi waliofaulu katika
daraja la kwanza hadi la tatu ni 23,520 na daraja la nne ni 103,327.
Watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 65.5 wamepata daraja 0,” alisema
Waziri Mkuu akiongeza: “Kutokana na matokeo haya mabaya, Serikali
imeamua kuunda tume hii itakayochunguza tatizo hili kwa madhumuni ya
kupata ufumbuzi wa kudumu.”
Alisema kuwa tume hiyo itakuwa na kazi nyingi
ikiwa ni pamoja na kubainisha sababu za matokeo hayo kuwa mabaya,
kutathmini nafasi za halmashauri katika kusimamia elimu ya sekondari na
kuainisha sababu nyingine zinazoweza kuchangia hali ya matokeo hayo.
“ Pia itapaswa kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua mara moja
kwa wanafunzi 240,903 waliopata daraja la sifuri katika Mtihani wa
Kidato cha Nne mwaka 2012, pamoja na kupendekeza jinsi ya kukabiliana
na mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu mara moja, kipindi cha muda
mfupi, kati na kipindi cha muda mrefu,” alisema Pinda.
Alisema pia tume hiyo itatathmini uwiano wa
mitihani inayotungwa na Baraza la Taifa la Mitihani, uhakiki wake na
maswali unaofanywa na Taasisi ya Elimu pamoja na kutathmini mihutasari
iliyotumika kuwaandaa wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne
mwaka 2012.
“Tume hii itachunguza pia umahiri wa walimu kumudu
maudhui wanayofundisha, mazingira ya kufundisha na kufundishia,
matumizi ya vitabu na zana za kufundisha na kujifunzia, pamoja na
utoshelevu wa walimu kwa masomo.
Kutathmini mchakato mzima wa usahihishaji na kuangalia usahihi wa alama za karatasi na majibu ya matokeo,” alisema Waziri Mkuu.
Mambo mengine ambayo tume hiyo inapaswa kuchunguza
ni pamoja na mwamko wa jamii kwenye elimu, upatikanaji wa chakula cha
mchana shuleni, kutathmini mikondo miwili mfumo uliopo Zanzibar na
kuangalia upungufu wa miundombinu, ikiwamo madarasa, maabara pamoja na
michango ya wazazi na walezi na kutathmini mfumo wa udhibiti wa nidhamu
ya walimu.
NA MWANANCHI
NA MWANANCHI
Post a Comment