Darren Bent akifunga bao kwa kichwa dakika za mwisho na kuipa timu yake matokeo muhimu hiyo jana Uwanja wa Old Trafford.
Darren Bent alifunga bao dakika za mwisho mwisho na
kumhakikishia kocha wao Rene Meulensteen matokeo muhimu wakati wa mechi
kati ya Fulham na Manchester United iliyochezwa katika uwanja wa Old
Trafford.
Fulham licha ya kushikilia nafasi ya mwisho
kwenye msururu wa ligi kuu ya Premier ilitoka sare ya kufungana magoli
mawili kwa mawili na mabingwa watetezi Manchester United.
Fulham
ndio iliyokuwa ya kwanza kuona lango la Manchester United, katika
kipindi cha kwanza kupitia kwa nahodha wake Steve Sidwell.
Hata hivyo wenyeji walijikakamua kipindi cha
pili ambapo walimiliki mpira kwa asilimia kubwa kabla ya Robin Van
Persie kusukuma kombora kali lililomuacha kipa wa Fulham kinywa wazi.
Dakika mbili baadaye Michael Carrick vile vile alivurumisha kombora lingine ambalo liliwaacha wachezaji wa Fulham wakishangaa.
Kadri muda ulivyoendelea kusonga mashabiki wa
Manchester United, walikuwa wameanza kusherehekea huku baadhi yao
wakimsifu kocha wao David Moyes.
Kama wahenga walivyonena, usikate kanzu kabla ya
mtoto kuzaliwa, uwanja wa Old Trafford ulitulia kama kaburi, pale
mchezaji wa ziada wa Fulham Daren Bent, alipofunga bao kwa kichwa baada
ya kipa wa Man United David De Gea kutema mkwaju wa Kieran Richardson.
Huzuni ilitanda katika uwanja wa Old Trafford
baada ya vijana hao wa Moyes kupoteza alama mbili muhimu na hivyo
kudidimiza matumaini ya United ya kuhifadhi kombe hilo au hata kumaliza
katika nafasi ya kwanza nne.
United ilifanya mashambulio mengi na wakati wa
mechi hiyo iliandikisha krosi 81, kiwango ambacho ndicho kubwa zaidi
kuwahi kuandikishwa na klabu yoyote tangu mwaka wa 2006.
United ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya
saba kwenye msururu wa ligi kuu ya Premier imepangiwa kutoana jasho na
Arsenal siku ya Jumatano na kocha David Moyes atakuwa na kibarua kigumu
kutuliza nyoyo za mashabiki wao.
CHANZO:BBC Swahili

Post a Comment