Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa hotuba yake huku wajumbe wengine wakisikiliza wakiwemo Mhe. Sofia Simba (Mb.), Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto(wa pili kulia). |
Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Mama Getrude Mongela aliyeongoza mkutano mkubwa wa wanawake miaka 20 iliyopita Jijini Beijing China. |
Tanzania
yatangaza hatua tano za kuendeleza haki za wanawake na usawa wa kijinsia
·
Yaahidi
kufanya mabadiliko makubwa ya kisera na kisheria
·
Miongoni
mwa Sheria zitakazohusika ni Sheria ya Ndoa na Sheria ya Urithi
·
Ni
katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu - SDG’s
Tanzania
imeahidi kuchukua hatua tano muhimu za kutetetea na kuendelea haki za wanawake kati
ya sasa na mwaka 2030, ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko makubwa ya kufuta
sheria zinazokandamiza wanawake na kutunga sheria za kuleta usawa wa kijinsia,
yote katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) mapya kwa
manufaa ya wanawake wa Tanzania.
Miongoni
mwa hatua hizo itakuwa ni pamoja na kufuta ama kufanya mabadiliko ambayo
yanaendeleza vitendo vya kiutamaduni ambavyo kwavyo vinaendeleza ubaguzi wa
wanawake kama vile Sheria ya Ndoa, Sheria ya Urithi na kutunga Sheria ya
Kukomesha Ukatili dhidi ya wanawake.
Msimamo
huo wa Tanzania umeelezwa Jumapili, Septemba 27, 2015 na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipozungumza katika Mkutano wa Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa
Akinamama: Dhamira ya Kuchukua Hatua uliohudhuriwa na wakuu wa nchi mbali mbali
duniani kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, Marekani.
Rais
Kikwete ameuambia mkutano huo ulioitishwa kwa pamoja na Jamhuri ya Watu wa China,
Denmark, Mexico na Kenya kuwa hatua ya pili ambayo Tanzania inakusudia kuchukua
ni kuridhia makubaliano yote ya kimataifa kuhusu haki za akinamama hasa
Makubaliano ya Kimataifa Juu ya Kukomesha Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya
Wanawake – Convention on the Elimination of All Forms of Discrimination Against
Women (CEDAW).
Hatua
nyingine ambazo Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania itachukua katika miaka 15
ijayo ili kuhakikisha usawa wa kijinsia nchini ni zifuatazo:
·
Kuendeleza na kuunga mkono upatikanaji wa
raslimali fedha zinazolenga kuongeza usawa wa kijinsia kwa mujibu wa Ajenda ya
Kugharimia Maendeleo ya Addis Ababa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinatolewa
pesa za kutekeleza mipango ya kitaifa na ya Serikali za mitaa za kukomesha
ukatili dhidi ya wanawake.
·
Kuhakikisha utekelezaji wa uwakilishi wa
uongozi wa asilimia 50-50 kati ya wanawake na wanaume katika nafasi zote za
maamuzi kwenye ngazi zote.
·
Kupatikana na kutumiwa kwa data na habari za
ukweli katika utunzi wa sera na utoaji maamuzi ya kukomesha ubaguzi wa kijinsia.
·
Kutunga na utekelezaji mfumo wa uwajibikaji na
ufuatiliaji wa haki za kijinsia na haki za akinamama zilizokubaliwa kitaifa na
kwenye ngazi ya Serikali za mitaa.
Rais
Kikwete pia amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuhusu hatua za kisera na
kisheria ambazo zimechukuliwa na Tanzania katika miaka ya karibuni kujenga
usawa wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 na
marekebisho yake ya mwaka 2004 ambayo yanawapa akinamama nafasi na haki ya kupata,
kushikilia, kutumia na kumiliki ardhi.
Hatua
nyingine ni kuwapa wanawake nafasi za maamuzi na uongozi katika nyanja za
kisiasa na maisha ya umma. Katika kutekeleza hilo, idadi ya wabunge wanawake
imeongezeka kutoka asilimia 21.5 ya wabunge wote mwaka 2005 hadi kufikia asilimia
34.5 mwaka huu, mawaziri wanawake wameongezeka kutoka sita mwaka 2005 hadi
kufikia 26 mwaka huu na idadi ya majaji wanawake imeongezeka kutoka wanane
mwaka 2005 hadi kufikia 41 mwaka huu.
Rais
Kikwete amesema kuwa hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni kupunguza
vifo vya wanawake wakati uzazi, kutunga Sheria dhidi ya ukatili wa kijinsia na
ukatili dhidi ya wanawake na watoto; kuanzishwa kwa uandaaji wa Bajeti
inayotilia maanani mahitaji ya wanawake na kuongeza uwezekaji wa kiuchumi wa
akinamama kupitia kuanzishwa kwa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) yenye kulenga
kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa akinamama wafanyao biashara ndogo ndogo na
za kati.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
28 Septemba, 2015
Post a Comment