| Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) | 
NA RAHMA SULEIMAN
Nyumba tisa zimeteketezwa kwa moto katika kisiwa cha Tumbatu Kaskazini 
Unguja muda mfupi baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kutangaza 
ushindi wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mgombea wa Chama
 Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.
Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, baadhi ya wafuasi na wanachama wa 
CCM kisiwani hapo walianza kushangilia ushindi huo. Hata hivyo, wakati 
wakiendelea kushangilia ushindi huo huku wakilidhihaki kundi lingine 
hali iliyosababisha warushiane mawe na mwishowe kuchomeana nyumba hizo.
Akizungumza na Nipashe, mmoja wa wananchi wa kisiwa hicho, Juma Ali, 
alisema kuwa wafuasi wa CCM waliokuwa wakisherehekea ushindi walikuwa 
wakiwazomea wafuasi wa wanaoaminika kuwa ni wa chama kingine na kuanza 
kupigana. 
Alisema ugomvi huo ulizusha taharuki hadi kufikia wafuasi hao wa pande 
mbili kuanza kurushiana mawe hadi kuchomeana moto nyumba zao za makaazi 
yao.
“Kwa kweli hali ilikuwa mbaya katika kisiwa hiki cha Tumbatu hasa kijiji
 cha Tumbatu Gomani ambacho kina wafuasi wengi wa CCM na kijiji cha 
Tumbatu Chwaka ambacho kina wafuasi wengi wa chama kingine,” alisema. 
Alifafanua kuwa nyumba zilizochomwa moto ni za Gomani na Chwaka.
Kamishana wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame, alisema 
jumla ya nyumba tisa katika kisiwa hicho zimechomwa moto na chanzo cha 
ugomvi huo ni matokeo ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa 
Tanzania kupitia CCM.
Alisema tayari polisi kwa kushirikiana na vikosi vya SMZ, vimeshatuliza 
ghasia hizo kisiwani humo na pia wanaendelea kufanya uchunguzi ili 
kubaini waliohusika na vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani.
CHANZO: NIPASHE
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Post a Comment