Simba ilikuwa imegeuka kibonde wa Kagera Sugar pamoja na timu za Tanga na Mbeya, lakini msimu huu imezigeuzia kibao.
Kocha mkuu wa Simba, Dylan Kerr.
Simba ililazimishwa sare na Mbeya City katika mechi zote mbili za
msimu wa kwanza (2013/14) wa timu hiyo ya Mbeya kushiriki Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara (VPL), kabla ya kuchezea kichapo katika mechi zote
mbili za msimu uliopita wa ligi hiyo, 2-1 nyumbani na 2-0 ugenini,
lakini juzi Wanamsimbazi walianza na kikosi chenye viungo watano, Said
Ndemla, Jonas Mkude, Abdi Banda, Mwinyi Kazimoto na Justice Majabvi na
kuchomoza na ushindi wa 1-0 dhidi ya timu hiyo mjini hapa.
Ushindi huo ni mwendelezo wa mabingwa hao mara 18 wa Bara kufanya
mabadiliko baada ya mwanzoni mwa msimu kuvunja mwiko wa kugawa pointi
kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kwa misimu mitatu, safari hii
wakichukua pointi sita kutoka kwa African Sports na Mgambo Shooting.
Mara tu baada ya kumalizika kwa mechi yao ya juzi jijini hapa,
kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola, aliiambia Nipashe kuwa Tanzania
Prisons ambao ambayo juzi ilisambaratishwa kwa kipigo kikubwa cha mabao
3-0 dhidi ya Stand United mjini Shinyanga, ijiandae kukumbwa na
mabadiliko ya Msimbazi keshokutwa.
"Tumecheza vizuri kipindi cha kwanza, kipindi cha pili hali ya hewa
ilitusumbua, lakini muhimu ni pointi tatu kwa sababu uwanja huu
(Sokoine) umekuwa mgumu kwetu kwa kipindi kirefu. Tuko hapa Mbeya kwa
ajili ya kuvunja mwiko na kupata pointi sita. Tayari tumepata tatu kwa
Mbeya City, tunazisubiri pointi tatu nyingine kutoka kwa Prisons
Jumatano," alitamba Matola.
Kuhusu mchezaji wa zamani wa Simba, Haruna Moshi 'Boban' ambaye
juzi alicheza kwa mara ya kwanza VPL akiwa na kikosi cha City, Matola
alisema: Hakuna asiyejua Boban ni mchezaji mzuri, tatizo linalomsumbua
kwa sasa ni kwamba amenenepa, lakini akifanya mazoezi, atawasaidia sana
Mbeya City."
Katika hatua nyingine, kocha mkuu wa Simba, Dylan Kerr, amekiponda
kikosi chake kwa kuonyesha kiwango duni kwenye mechi yao ya juzi dhidi
ya City.
Katika mahojiano na Nipashe jijini hapa jana, Muingereza huyo
alisema: "Sijafurahishwa na namna timu ilivyocheza dhidi ya Mbeya City.
Tulizidiwa kwa kiasi kikubwa, goli na ushindi pekee ndicho kitu cha
kufurahia hapa, hatukucheza hivi kwenye mazoezi. Mechi haikuwa na furaha
kwangu kwa sababu tumecheza soka la Amerika."
Kocha wa Mbeya City, Abdul Mingange, aliliambia gazeti hili jijini
hapa juzi kuwa ili timu yake ifanye vizuri VPL msimu huu, watalazimika
kusaka washambuliaji wakali wakati wa usajili wa dirisha dogo mwezi
ujao.
"Tumetengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini safu yetu ya
ushambuliaji imetuangusha. Tunatakiwa kulitumia vyema dirisha dogo
kuongeza washambuliaji," alisema meja huyo mstaafu ambaye msimu uliopita
alikinoa kikosi cha Ndanda FC ya Masasi, Mtwara.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment