Vyama vinavyounda UKAWA.
Hadi kufikia jana, tayari muungano huo unaoundwa na vyama vya
NCCR-Mageuzi, NLD, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), ulishapata madiwani wengi na hivyo kujihakikishia
utawala katika halmashauri za wilaya, miji, manispaa na jiji katika
mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Mtwara, Mbeya, Lindi, Kagera na Arusha.
MTWARA
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa hadi sasa, CUF na Chadema
tayari zimejihakikishia utawala katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara
Mjini baada ya kutwaa jumla ya kata 11 dhidi ya 7 za Chama Cha
Mapinduzi (CCM). Kati ya hizo, CUF imeshinda kata 8 na Chadema kata 3.
Awali, CCM ndiyo waliokuwa wakiongoza halmashauri hiyo.
Kadhalika, CUF pia imetwaa utawala wa Halmashauri ya Wilaya ya
Tandahimba baada ya kushinda katika kata 20 kati ya 31 zilizopo, Chadema
wakipata kata moja na nyingine 10 zikiangukia CCM. Aidha, CUF
wameshinda pia ubunge katika majimbo hayo mawili ya Mtwara Mjini na
Tandahimba.
ARUSHA
Katika mkoa wa Arusha, matokeo yanaonyesha kuwa hadi sasa Chadema
wanaongoza katika halmashauri za wilaya za Monduli, Jiji la Arusha,
Arumeru Mashariki na Arumeru Magharibi.
Halmashauri ya Jiji la Arusha, Chadema imeshashinda katika kata 24 na CCM kuambulia kata moja.
Arumeru Mashariki, Chadema imepata kata 25 na CCM kata sita,
Arumeru Magharibi Chadema kata 21 na CCM sita huku Monduli Chadema
ikipata kata 15 na CCM kata 5. Na kote huko, Chadema imetwaa pia viti
vya ubunge.
TANGA
Licha ya kutwaa ubunge wa Jiji la Tanga, CUF pia imetwaa utawala wa
Jiji hilo baada ya kushinda katika kata 11 dhidi ya CCM iliyoambulia
kata 5.
MBEYA
Katika mkoa wa Mbeya, tayari Chadema ina uhakika wa kuongoza
Halmashauri ya Jiji la Mbeya na pia Halmashauri ya Mji wa Tunduma
wilayani Momba.
Matokeo yanaonyesha kuwa katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya lenye
kata 36, Chadema imepata kata 26 huku CCM ikipata kata tisa na kata moja
uchaguzi ukiahirishwa kufuatia kifo cha mgombea wa CCM wakati wa
kampeni.
Kabla ya uchaguzi wa mwaka huu, Halmashauri ya Jiji la Mbeya
ilikuwa ikiongozwa na CCM iliyokuwa na madiwani 22 huku Chadema ikiwa na
madiwani 12 na wengine wawili wakiwa wa NCCR Mageuzi.
Katika Jimbo la Tunduma, Chadema imeshinda kata 14 huku CCM ikiambulia kata moja kati ya 15 zilizopo.
KAGERA
Chadema na washirika wake Ukawa wamefanikiwa kutwaa Manispaa ya
Bukoba baada ya Chadema kushinda katika kata 7, NCCR moja na CUF kata
moja huku CCM ikipata kata 5
IRINGA
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Chadema ilishapata kata
18 hadi kufikia jana mchana na CCM kupata kata 4, hivyo kujihakikishia
utawala katika halmashauri hiyo.
KILIMANJARO
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Chadema iliyovuna wabunge sita na
NCCR-Mageuzi yenye mbunge moja katika mkoa wa Kilimanjaro, sasa zitaunda
Halmashauri tano za Wilaya ambazo ni Moshi Mjini, Hai, Siha, Rombo,
Moshi Vijijini na Vunjo; wakati CCM ikiwa imeambulia Halmashauri mbili
za Mwanga na Same.
Majimbo hayo na idadi ya Kata ambazo Chadema na NCCR-Mageuzi
zitaunda Halmashauri zake ni Moshi Mjini, Chadema imeshinda Kata 19 kati
ya 21 na CCM imepata Kata mbili za Bondeni na Kilimanjaro, wakati jimbo
la Hai, Chadema imeshinda Kata 16 kati ya 17, ambapo Kata moja ya
Bomang’ombe ndio pekee haijafanya uchaguzi kutokana na mgombea wa CCM
kufariki dunia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Aidha, Chadema iliyoshinda Kata 27 kati ya 28 za Wilaya ya
Rombo,ndiyo itakayounda Halmashauri ya Wilaya hiyo, huku NCCR-Mageuzi
iliyoshinda Kata nane, kati ya 16 na Chadema iliyoshinda viti 15 vya
udiwani katika jimbo la Moshi Vijijini, sasa zitaunda Halmashauri moja
ya Wilaya ya Moshi. Katika jimbo la Moshi Vijijini CCM imeshinda Kata
moja.
LINDI
Katika mkoa wa Lindi, CUF imefanikiwa kupata uongozi wa halmshauri
za wilaya za Kilwa ambako imetwaa kata 8 kati ya 10 za Kilwa Kusini na
pia halmashauri ya Wilaya ya Liwale ambako imepata kata 14 huku CCM
ikipata kata 6.
MARA
Chadema imetwaa kata 4, sawa na CCM, huku ikitwaa utawala Tarime Vijijini baada ya kushinda katika kata 16 dhidi ya 10 za CCM.
*Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Godfrey Mushi, Juma Mohamed, Emmanuel Lengwa na Daniel Mkate
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment