Na Gabriel Ng’osha
HATIMAYE mwenyekiti wa CUF aliyejiuzulu,
Profesa Ibrahim Lipumba (pichani) ameibuka na kumgeukia rais wa awamu
ya tano, Dk. John Pombe Magufuli ambaye anatarajiwa kuhutubia Bunge leo
kwa kumuambia kuwa ana mzigo mzito kutokana na hali ngumu ya bajeti ya
nchi.
Akizungumza jana na wanahabari katika
ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar, Profesa Lipumba
alisema Rais Magufuli anakabiliwa na mambo kadhaa yakiwemo ya hali ngumu
ya bajeti ya serikali kufuatia taarifa (iliyopo kwenye tovuti) ya Benki
Kuu ya Tanzania kuonesha kuwa mwaka wa fedha 2014/2015 serikali
ilipanga kukusanya mapato ya ndani ya shilingi bilioni 12,178, sehemu
kubwa ikiwa ni makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na badala
yake serikali ilikusanya shilingi bilioni 10,507.
Rais Dk. John Pombe Magufuli.
Alisema mapato halisi ni madogo
ukilinganisha na bajeti kwa kiasi cha shilingi bilioni 1,671 sawa na
asilimia 14 ya malengo ya bajeti ya serikali.
Aliongeza kuwa halmashauri za wilaya,
miji na majiji zilitarajiwa kukusanywa shilingi bilioni 458.5 lakini
zilifanikiwa kukusanywa shilingi bilioni 360.1 sawa na asilimia 78. ya
malengo ya bajeti.
Kwa upande wa misaada, Profesa Lipumba
ambaye ni mtaalam wa uchumi alisema kuna bajeti ya shilingi bilioni
1,481 lakini zilitolewa shilingi bilioni 1,024, upungufu ukiwa ni
shilingi bilioni 457 sawa na asilimia 31 ya bajeti huku mikopo yenye
masharti nafuu ya shilingi bilioni 1,000 ikafanikiwa kwa kupatikana
shilingi bilioni 859.
Akizungumzia Tume ya Uchaguzi ya Zanziba
(Zec), Lipumba amemtaka Rais Magufuli kutumia uamiri jeshi wake mkuu
kuzungumza na kuishauri Zec kumtangazab mshindi wa urais na siyo kurudia
uchaguzi kama serikali ya CCM Zanzibar inavyotaka.
“Kila kitu kiko wazi, mawakala walipata
nakala za kila jimbo kwa majimbo yote 54, binafsi namuomba Rais Magufuli
aishauri Zec itangaze matokeo halisi,”alisema Lipumba.
Aliongeza kuwa kwa kasi ya Rais Magufuli
naungana naye katika kauli mbiu yake ya “Hapa Kazi Tu”, lakini alimtaka
azingatie kauli nyingine ya “HAPA HAKI TU’’ili kuinusuru nchi isiingie
kwenye machafuko yasiyo na msingi.
“Nampongeza kwa ziara zake za
kushtukiza, tumeona zinazaa matunda mfano mzuri ni Hospitali ya
Muhimbili baada ya kufika pale mashine za CT Scan na MRI zilitengemaa
lakini ziara hizo hazitakuwa na tija kama bajeti ya maendeleo haikidhi
matatizo ya Watanzania kama vile afya bora, elimu, ajira, kupambana na
rushwa, miundo mbinu na kilimo ili kuwe na chakula cha kutosha nchini.
Aidha, Lipumba amempongeza Waziri Mkuu Mteule, Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na Bunge kumpitisha.
“Naweza kusema Majaliwa ni kama kaokota
embe dodo chini ya mpapai, Rais Magufuli hajakosea sana kwani yeye ndiye
kiongozi na mtendaji mkuu, hivyo aliyeteuliwa anafaa kufanya naye kazi
kwa karibu zaidi. Ingawa inampasa ajenge uwezo mkubwa sana wa kuwaongoza
na kuwakabili wabunge pamoja na baadhi ya vigogo ambao nao walikuwa
wanategemea wachaguliwe uwaziri mkuu,” alisema.
Post a Comment