NA MWINYI SADALLAH
12th November 2015
12th November 2015
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekifungia kituo cha Radio
Swahiba FM kurusha matangazo yake, baada ya kutangaza matokeo aliyotoa
mgombea urais wa Zanzibar kupitia Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad
(pichani), akidai alikuwa mshindi katika uchaguzi uliyofanyika Oktoba
25, mwaka huu visiwani humo.
Uamuzi wa kufungiwa kituo hicho cha radio ulitolewa jana na Katibu
Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Chande Omar, kupitia barua ya
Novemba 11, mwaka huu.
“Tume kwa kuzingatia uungwana uliotumia wa kukiri kosa na baada ya
kupitia maombi yako kwa mujibu wa kifungu cha 16(3) na kifungu 3(F)
imetoa tahfifu ya kutopokonywa leseni na badala yake kufungiwa hadi
Januari 13, mwaka,” ilisema barua hiyo kwenda kwa kituo hicho cha radio.
Chande alisema pamoja na adhabu hiyo, mmiliki wa kituo hicho
anatakiwa kueleza kwa maandishi kuwa kituo chake hakitarudia tena kosa
kama hilo au jingine linaloweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini.
Alisema iwapo kituo hicho kitashindwa kujirekebisha pamoja na kupewa
adhabu hiyo kwa kutumia kifungu cha 16 cha Sheria ya Tume ya Utangazaji
ya Mwaka 2007, adhabu kali itachukuliwa.
Barua hiyo nakala yake imetumwa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni,
Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk, aliyetangaza kujivua wadhifa wake
kwa madai ya serikali awamu ya saba imefikisha kikomo cha kuendelea
kubakia madarakani Novemba 2, mwaka huu.
Nakala nyingine imetumwa kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ali
Mwinyikai, pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Utangazaji Zanzibar,
Abdalla Mwinyi Khamis.
Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugezi wa Radio Swahiba FM, Khasim
Suleiman, alisema wafanyakazi 24 wa kituo hicho na familia zao
wameathiri kutokana na uamuzi huo wa serikali wa kukifungia kituo hicho.
Alisema walifanya juhudi mbalimbali za kufanya mazungumzo na tume
lakini ghafla jana walipokea barua ya kufungiwa hadi Januari 13,
mwakani.
Radio Swahiba FM ilirusha matangazo ya moja kwa moja Oktoba 26, mwaka
huu, kwenye mkutano na waandishi wa habari wa Maalim Seif ambaye alidai
kuwa ameshinda nafasi ya urais wa Zanzibar kwa asilimia 52.87 dhidi ya
mpinzani wake Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (CCM) aliyepata
asilimia 47.13 katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment