David Kafulila alipokuwa bungeni.
...........................
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na vyama vya upinzani kuweka
mbele mapambano dhidi ya ufisadi ndani ya serikali kuanzia awamu ya pili
uongozi wa nchi chini ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi.
Katika kipindi hicho chote wapinzani waliendelea na mapambano hayo
na kuyafanya ajenda ya kudumu kwa serikali ya awamu ya tatu ya Rais
mstaafu Benjamin Mkapa na awamu ya nne ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Ni mapambano mazuri ambayo yalisaidia kuikumbusha serikali hizo
dhidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma hapa nchini.
Sasa tupo katika uongozi wa awamu ya tano ya Rais John Magufuli
ambaye amekuja na kauli mbiu ya 'kutumbua majipu' ikiwa ni namna ya
kipekee ya kupambana na ufisadi.
Anafanya hivyo baada ya kukiri kwamba alikuta uozo mkubwa ndani ya
serikali na kwamba ni kazi kubwa kutumbua majipu na anahitaji Watanzania
wamuombee kwa Mungu.
Ametangaza kujitoa sadaka ili kuikomboa nchi hii dhidi ya vitendo viovu vya ufisadi.
Moja ya wapinzani ambao wamekuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi hadharani ni mwanasiasa kijana, David Kafulila.
Kafulila ambaye alikuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) kati
ya 2010 hadi 2015, anasema juhudi za Rais Magufuli zinapaswa kuungwa
mkono na watu wote.
Mwanasiasa huyo akizungumza katika mahojiono maalum anasema,
wazalendo wote wanapaswa kumuunga mkono kwa sababu mapambano haya
yanaleta nidhamu ya utendaji serikalini.
Anasema kwa muda mrefu serikali zote zilikuwa katika hali mbaya
katika nidhamu ya utendaji ambao ulitokana na kuwapo mfumo mbovu.
Kikubwa anachokisema Kafulila ni kujenga mfumo imara ambao
utasimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma hata kama Rais Magufuli
atamaliza kipindi chake na kuondoka.
"Rais anatakiwa ajenge mfumo unaotisha ili hata asipokuwapo kwa
sababu yoyote ile nchi ibakie na nidhamu ya utendaji kazi na hofu ya
ufisadi.
Kafulila anasema panapokuwa na mfumo mzuri wa utendaji kazi hata
kiongozi mwingine anapokuja lazima atabanwa ili afanye hiki
kinachofanywa na Rais Magufuli kwa sasa.
Hata hivyo, Kafulila anasema Rais Magufuli anapaswa kutambua kuwa
hofu ya sasa ni ya muda mfupi kwani anaogopwa yeye na sio mfumo.
Anasema kuwa njia pekee ya kuhakikisha hilo linatendeka ni pamoja
na kuwapo kwa katiba mpya itakayojenga mifumo thabiti katika utendaji
kazi.
“Zaidi anapaswa kuruhusu demokrasia hasa ya Bunge ili limsaidie kutumbua majipu kwani peke yake hawezi,” anasema Kafulila.
SAKATA LA UFISADI WA KASHFA YA ESCROW
Kafulila ambaye alijinyakulia umaarufu bungeni baada ya kuibua
tuhuma nzito akiwahusisha mawaziri wawili kuhusika katika uchotwaji wa
fedha zaidi ya bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa
inamilikiwa kwa pamoja kati ya Shirika la Umeme (Tanesco) na kampuni ya
kufua umeme ya IPTL.
Kuhusu sakata la Escrow anasema anachokiona kwa Rais Magufuli bado anaivutia pumzi.
”Simuoni akiigusa ingawa sioni akiicha iendelee,” anasema Kafulila.
Anasema anachokifanya kwa sasa ni kuhangaika na kesi yake ya
kupinga ushindi alioupata mgombea wa CCM katika jimbo la Kigoma Kusini
mwaka jana.
Anakiri kwamba alikuwa mwiba mkali kwa serikali ya Kikwete na
kwamba bado anawaza kuendelea na juhudi hizo za kupinga ufisadi
hadharani.
Mwanasiasa huyo kijana anasema kinachofanywa na Rais Magufuli
hususani kuwafukuza wezi wa fedha za umma kwa sasa mtu anaweza kudhani
Ikulu haikuwa na Rais miaka mitano iliyopita.
Akizungumzia uchaguzi wa mwaka jana, Kafulila anasema ulikuwa na
ushindani mkali ambao haujawahi kutokeo katika chaguzi zote zilizowahi
kufanyika nchini.
Kafulila anasema ushindani huo ulikuwa ni jaribu kwa mfumo kuona
kama upo imara kusimamia uchaguzi wa ushindani kuanzia ngazi ya
Udiwani, Ubunge na Urais.
“Jambo moja kubwa nililoliona ni udhaifu wa mfumo hasa kuanzia kwa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kunahitajika mabadiliko ya kikatiba
kwa sababu kwa kiasi kikubwa hii ni Tume ya serikali na siyo ya umma,”
anasema Kafulila.
Anasema mfumo unaifanya iwe hivyo kwamba wasimamizi wote wa
uchaguzi kwenye majimbo ambako kunaamua nani awe mbunge na diwani na
hata Rais ni watendaji kata na wakurugenzi ambao hakika ni sehemu ya
Tamisemi ambao ni serikali.
“Sheria inasema wasimamizi hao wa uchaguzi ndiyo wenye kauli za
mwisho katika kumtangaza mshindi, na baada ya hapo labda mtu aende
mahakamani," anasema Kafulila.
Anatoa mfano kwamba kama NEC ingekuwa kwa ajili ya wananchi
ingeweza kutatua migogoro mingi ya uchaguzi na kuimaliza na isingeenda
mahakamani.
Kafulila anatoa mfano kuwa kuna wagombea wanalalamika kwamba
alitangazwa mshindi ambaye hakushinda na fomu za matokeo zinaonyesha
hivyo na kwamba jambo kama hilo lingepaswa kuishia kwa Tume kwa mfumo
wa rufaa na kurekebisha kasoro kama hizo.
Anasema masuala ya kufikishana mahakamani yangebaki yale ambayo yanayohitaji sayansi kubwa kutambua haki ni ya nani.
Kafulila alishauri kuwa serikali iondolewe kwenye mfumo wa Tume ili
iajiri watu wake watakaowajibika kwa yenyewe na siyo kuwa na watumishi
wanaowajibika kwa serikali.
NAFASI YA VYAMA VYA UPINZANI KWA SASA.
Akizungumzia nafasi ya upinzani kwa sasa anasema kuwa bado upinzani
una nafasi kubwa hasa ukizingatia kuwa Rais Magufuli ameeleza yupo
tayari kujiuzulu urais kama akishindwa kupambana na ufisadi.
Anasema hoja ya ufisadi ni ya upinzani kwa miaka mingi, hivyo
nafasi ya upinzani bado ipo hususani kumuelekeza Rais yalipo majipu.
“Jambo la msingi ni Rais asimamie kwa dhati kauli yake kuwa yeye ni
rais wa wote bila kujali itikadi za siasa, dini, rangi wala ukanda
na kikabila kwani itamsaidia kujenga uwajibikaji,” anasema.
Aliongezea kuwa “Rais aone upinzani ndiyo ustawi wa taifa lake,
kwani hata yeye, asingepewa nafasi ya kugombea kupitia CCM kama CCM
isingehofu upinzani.
Alionekana kama mtu anayeweza kukabili wimbi la mabadiliko ili
kuinusuru CCM ndio sababu akapewa siyo kwamba wenye CCM walimpenda,”
anasema Kafulila.
Kuhusu serikali ya sasa ya CCM kama imekidhi kiu ya upinzani kwa
kile walichokuwa wanakililia kwa miaka mingi, Kafulila anasema kuwa bado
ni mapema kusema haya.
“Bado hata mwaka haujamalizika siasa zinaendelea tena kwa kasi,
hata serikali ifanye nini upinzani utazidi kukua kwani unaweza kubadili
mbinu ndiyo maana nchi zenye maisha bora duniani kama Finland bado kuna
upinzani mkali,” anasema Kafulila.
MAISHA YAKE KISIASA BAADA YA KUSHINDWA UBUNGE
Kafulila anasema yeye bado ni mwanachama halali wa NCCR-Mageuzi na pia ni Katibu mwenezi Taifa.
“Sijui habari za kuhama NCCR msingi wake ni nini, kwa sasa nipo
mahakamani nashughulika na kesi ya ubunge wangu hilo ndilo jambo kubwa
naweza kusema hayo mengine sina nafasi kuyazungumzia,” anasema Kafulila.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment