Je,
Falsafa ya Kuanzishwa kwa Mbio za Mwenge wakati wa Uhuru wa Tanganyika
tarehe 9/12/1961 imepitwa na wakati??? Je, kuna wakati utafika misingi
ambayo taifa hili lilijengwa kwahiyo, itapitwa na wakati? Je, tuachane
na mbio za Mwenge kwa sababu za gharama kuwa kubwa - wengine wanasema
mwenge ni Jipu na Rais Magufuli alitumbue? Au Mbio za Mwenge zina
umuhimu na ni sehemu ya msingi ambao taifa hili lilianzishwa na ni
kumbukumbu ya mapambano ya kumletea mabadiliko na maaendeleo Mtanzania?
Yote haya nitayatolea ufafanuzi kwenye Penyenye Fupi Fupi.
Falsafa
ya Mwalimu Julis Kambarage Nyerere kuhusu mwenge wa Uhuru ilikuwa ni:
“Sisi Watanganyika, tunataka kuuwasha Mwenge na kuuweka juu ya mlima
Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo
hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa
dharau”.
Je,
Falsafa ya Kuanzishwa kwa Mbio za Mwenge wakati wa Uhuru wa Tanganyika
tarehe 9/12/1961 imepitwa na wakati??? Ikumbukwe kwamba falsafa hii ni
sehemu ya misingi ya Taifa letu..tangu ilipoanzishwa na waasisi wetu.
Mataifa yaliyoendelea yameendelea kuenzi misingi iliyojenga Mataifa hayo
kwa gharama zozote zile. Tutakubaliana sote kuwa Watanzania bado
tunahitaji kujikwamua kutoka kwenye ujinga, maradhi, na umaskini.
Tunahitaji kujikwamua kutoka kwenye dhuruma na chuki ambazo, ukizingatia
dhana ya mazingira na wakati, zimekuwa ni tofauti zaidi ukilinganisha
na wakati wa Uhuru. Japokuwa wakati wa Uhuru kulikuwa na dhuruma,
ufisadi, chuki nakadharika, bado hata sasa hivi tuna ufisadi, dhuruma na
chuki tena zilizoenda mbali sana. Katika dhama hizi za Magufuli,
zilizotofauti kabisa na nyakati za Kikwete, Mkapa, Mwinyi na zile za
wakati wa Baba wa Taifa. Tumejionea uozo wa hali ya juu kuliko ambavyo
tumewahi kushuhudia. Neno hili siyo geni tena kwetu – “Tanzania ilikuwa
ni shamba la bibi”. Mwenge wa Uhuru unapaswa kutukumbusha kila mara
kuwa vita dhidi ya ubadhirifu, chuki, na dharau bado inaendelea. Tena
falsafa ya Mwalimu ilikuwa inataka huu Mwenge umulike hadi nje ya mipaka
yetu. Hii inanipeleka kwenye penyenye yangu inayofuata – Kuingiliwa kwa
Uhuru wa Taifa letu na Mataifa ya Magharibi.
Tutakumbuka
kuwa hivi karibuni sakata la MCC 2 lilishika kurasa nyingi sana. Baada
ya Uchaguzi Mkuu wa Marudio wa Zanzibar na kuhusiana na ile sharia ya
makosa ya Kimtandao. Taasisi ya MCC ni kibaraka wa umagharibi, pia ina
kila lengo la kuingilia mambo ya ndani ya nchi yetu. Maitaifa ya
Magharibi kuingilia mambo ya ndani ya nchi za kiafrika limekuwa ni jambo
la kawaida sana. Tumekuwa ni nchi ya amani isiyokiuka haki za binadamu,
sasa kuiingiliwa kwenye mambo ya ndani ya nchi ni jambo linakiuka hadhi
yetu ya kuwa Sovereign State. Mwenge wa Uhuru unatukumbusha maneno ya
Mwalimu Julius Nyerere kuwa “… tunataka kuuwasha Mwenge na kuuweka juu
yam lima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu...” Je msingi huu
wa kuanzishwa kwa Taifa letu umepitwa na wakati, hasha.. msingi huu bado
uko na unaendelea. Na kama taifa lazima tusimame kidete. Mwenge huu
inabidi tuumulike ili sisi kama Watanzania tujikumbushe, na hayo mataifa
ya nje yaliyo karibu nasi na yaliyo Magharibi au Mashariki. Pia
ninaungana na kauli ya Mh. Rais Dk. John Joseph Magufuli kuwa ni bora
kuishi kwa kula mihogo kuliko kula mkate ya masimango.
Je, kuna wakati utafika misingi ambayo taifa hili lilijengwa kwayo, itapitwa na wakati?
Mwalimu
Julius Nyerere, alipohutubia Watanganyika kwa mara ya kwanza kama
Waziri Mkuu wa Tanganyika, alielekeza kuwa Tanganyika iko vitani dhidi
ya ujinga, maradhi na umaskini. Ni nukuu baadhi ya maneno yake:
“…matatizo haya, hayanitishi mimi, hayawatishi wenzangu, na wala
hatuombi kwamba yawatisheni ninyi. Tunayaona kwamba ni jaribio tu…Mara
nyingi sana, nimesema nayi juu ya umaskini, ujinga, na maradhi, lakini
kwa kweli adui yetu mkubwa ni umaskini. Tukiweza kumshinda adui huyu,
tutakuwa tumeweza kupata silaha itakayotuwezesha kuushinda ujinga na
maradhi. …tunaweza kupigana vita vya umaskini. Namuomba kila raia wa
Tanganyika, aape kiapo cha kuwa adui wa umaskini. Amshambulie adui huyo
mahali popote atakapoonekana.”
Japokuwa
Tanganyika ilipata Uhuru wake bila mapambano dhidi ya mkoloni
yaliyohusisha kumwaga damu. Msingi tuliachiwa na Baba wa Taifa ni kuwa
nchi iko kwenye mapambano dhidi ya umaskini. Kila Mtanzania anapaswa
kuwa vitani wakati wowote. Nikiiweka hoja hii kwenye muktadha wa Mwenge
wa Uhuru ambao unajengwa kwenye msingi wa kumulika ubadhirifu na
dhuruma. Tumeshuhudia ambavyo viongozi au watumishi wetu katika kada
mbalimbali wakiwa mstari wa mbele kwenye ubadhirifu wa mali za umma.
Kuingia mikataba isiyokuwa na tija wala maslahi ya Taifa. Watu hawa
wamekuwa wakiturudisha nyuma sana kwenye vita dhidi ya umaskini ambao
mwalimu alitutaka kila Mtanzania kuapa kupambana nao kila sehemu
atakapoukuta. Ila katika juhudi za Mtanzania maskini kujitafutia njia za
kutoka kwenye umaskini na wengine kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi,
wachumia tumbo wamekuwa na mtindo wa kujinufaisha wao na vizazi vyao.
Kinyume kabisa na misingi ya Taifa letu. Kila Mtanzania akiwa vitani
dhidi ya umaskini inamaanisha kuwa atafanya kazi kwa bidii ili kujipatia
kipato na serikali itatimiza wajibu wake kuwaletea wananchi bidhaa za
umma. Ndiyo maana katika dhama hizi za Magufuli utumbuaji wa majipu
unaturudisha kwenye ile vita dhidi ya dhuruma, ufisadi, na uonevu.
Mwenge lazima uendelee kumulika, falsafa na itikadi ya kuwa tuko katika
mapambano lazima iendelee kumulikwa.
Je,
tuachane na mbio za Mwenge kwa sababu za gharama kuwa kubwa - wengine
wanasema mwenge ni Jipu na Rais Magufuli alitumbue? Au Mbio za Mwenge
zina umumhimu na ni sehemu ya msingi ambao taifa hili lilianzishwa kwayo
na ni kumbukumbu ya mapambano ya kumletea mabadiliko na maaendeleo
Mtanzania?
Kama
nilivyelezea hapo juu nia, falsafa na matokeo ya kuwepo kwa mbio za
Mwenge wa Uhuru bado hazijabadilika. Changamoto ambazo zilikuwepo wakati
wa Uhuru wa Tanganyika, bado zipo katika kipindi cha Tanzania ya karne
ya 21, na inawezekana Tanzania ya vizazi vijavyo itakutana na changamoto
zinazofanana na hizi lakini kadika mazingira na wakati wa vizazi vya
wakati huo.
Kama
Taifa misingi ya kuanzishwa kwa Taifa lazima iendelezwe, kwani
wanaosema kuachana na misingi hiyo huwezi fahamu ajenda yao iliyojificha
ni mimi. Taifa lisilo na misingi ya kuanzilishwa kwake ni dhaifu. Taifa
linaloweza kutupilia mbali misingi ya kuanzilishwa kwake, linaweza kuwa
katika hatari kubwa sana ya siku moja kutoweka, au kuingia katika
virugu na matatizo ambayo ni vigumu kuweza kurudi katika hali ya awali.
Bado tunaihitaji misingi ya Taifa letu. Bado tunaipenda misingi ya Taifa
letu. Gharama ya mbio za Mwenge siyo hoja, maana misingi ya kuanzishwa
kwa Taifa lazima ilindwe kwa gharama zozote zile. Ufisadi uliokuwa
unaendana na kukimbiza mbio za Mwenge wa Uhuru ndiyo unaotakiwa kupigwa
vita kwa juhudi zote. Mwenge kwa sababu unamulika na kuangaza palipo na
ufisadi, udharimu, dharau, na chuki. Mbio za Mwenge wa Uhuru zitumike
kutumbulia kila linapokuwa limemulikwa jipu, kwenye miradi ambayo
imekuwa ni utamaduni kutumika kuizindua nchi nzima yaani mikoa 31 na
Halimashauri 173.
Kumbukumbu
ya kumletea Mtanzania mabadiliko ya kiuongozi na uundwaji wa mfumo wa
utawala bora utakao ridhishwa kizazi hadi kizazi, ni jambo linalopaswa
kuwa sehemu ya ujivuni wa kuwa na Mwenge wa Uhuru. Mwenge ni alama ya
Uhuru wetu kuona mapungufu yetu. Mwenge ni alama ya kutuunganisha
Watanzania na kupambana na uovu, udharimu, wizi, na ufisadi. Mwengi ni
alama ya Uzalendo na kila Mtanzania nia akiuona anapaswa kuukumbuka
wakati wa uhai wake wote, na kuwafundisha watoto na watoto wa watoto
wake kuwa hiyo ndiyo ishara ya Uzalendo wa Mtanzania. Ndiyo ishara la
tumaini la Mtanzania lilioanza tangu na kabla baada ya kupata Uhuru na
lilikuwepo kabla ya kupata Uhuru. Wanaoupiga vita Mwenge wa Uhuru
wamepoteza tumaini na wanataka Watanzania nia pia wapoteze tumaini
pamoja nao. Ninachoamini mimi ni kuwa mtu aliyepoteza tumaini safari
yake inapaswa kuishia kaburini. Tena kwa sisi tuliona tumaini la kizazi
hiki na kutambua ukuu wa Mungu, tunaamini hata baada ya Kaburi
tunatumaini kuwa siku moja tunauna uso wake. Sasa iweze sisi Watanzania
tukubali mawazo haya finyu kuwa Mwenge ni Jipu, ninadhani kupoteza
Tumaini ni Jipu, na dawa ya jipu ni kulitumbua na Mwenge unamwangaza kwa
kutosha kumulika wakati wa Utumbuaji wa Jipu hilo.
Mnyela Jonathan N.
Post a Comment