Maskini wee! Baba wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond
Platnumz’, Abdul Juma ‘Baba D’ anaumwa sana! Ndivyo Risasi Mchanganyiko
linavyoweza kukuhabarisha baada ya mzazi huyo kuzidiwa ghafla na
kukimbizwa hospitalini kutibiwa kwa msaada kutokana na kukosa fedha,
twende hatua kwa hatua.
NI JUMAPILI ILIYOPITA
Tukio hilo la kusikitisha la baba mzazi wa msanii ambaye anatajwa kuwa
na ukwasi wa kutosha Bongo, lilijiri Jumapili iliyopita ambapo kwa
msaada wa Dk. Fadhili Emily wa Kituo cha Tiba cha Fadhaget Sanitarium
kilichopo Mbezi Beach-Africana, Dar, baba Diamond alifikishwa kutoka
nyumbani kwake Magomeni-Kagera hadi hospitalini hapo na kupatiwa
matibabu.
CHANZO CHAVUJISHA
Awali, Risasi Mchanganyiko lilipokea taarifa za mzee Abdul kuzidiwa
nyumbani kwake lakini ikaelezwa kwamba, hakuwa na msaada wowote hadi
majirani walipopata mawasiliano ya daktari huyo na kumuomba amsaidie.
“Jamani baba D (baba Diamond) yupo hoi hapa nyumbani kwake Magomeni.
Miguu inamuuma, anashindwa kutembea na ukizingatia hana kipato,
anashindwa pia kwenda hospitali. Na bahati mbaya kwa muda mrefu hata
majirani wamekuwa wakimsaidia lakini bado hajapata tiba sahihi.”
AUNGANISHWA NA DK. FADHILI
“Leo (Jumapili) kuna jirani yake mmoja hapa ndiyo amepata wazo baada ya
kusoma Gazeti la Risasi Jumamosi (ndugu na hili), amepata namba za Dk.
Fadhili katika makala anazoandika gazetini kuhusu afya. Akampigia na
kumuomba msaada na bahati nzuri dokta huyo ameguswa na tatizo la mzazi
huyu, amemtumia nauli ya teksi ili akimbizwe hospitalini kwake, sasa
hivi ndiyo wanaelekea huko,” kilisema chanzo hicho.
MAKACHERO WAUNGA TELA
Licha ya kuwa muda huo ulikuwa umeyoyoma (saa 1 usiku), makachero wetu
waliingia mzigoni kuelekea moja kwa moja Mbezi kwenye hospitali hiyo na
kumkuta baba D akiwa anaingia mapokezi katika kliniki hiyo.
ASAIDIWA NA WAHUDUMU
Akiwa mapokezi, makachero wetu walimshuhudia baba Diamond akisaidiwa na
vijana wawili ambao ni wahudumu wa hospitali hiyo, walimkalisha kwenye
kochi kisha wakaanza kumpa huduma ya dharura ambapo walimpima presha na
kumuita Dk. Fadhili atazame miguu yake.
KUHUSU MIGUU
Dk. Fadhili alipofika, alimvua soksi baba huyo na kuikagua vizuri miguu
hiyo kabla ya kuingia naye ndani katika chumba maalumu cha vipimo na
matibabu.
VIPIMO VINGINE
Ilibainika kuwa, miongoni mwa vipimo alivyopimwa baba D ni pamoja na
kile cha Quantum Magnetic Analyzer ‘QMA’ ambacho kazi yake ni kutambua
magonjwa mbalimbali ndani ya mwili wa binadamu. Hata hivyo, Risasi
Mchanganyiko halikufanikiwa kujua kipimo hicho kilitambua nini!
BABA DIAMOND AFUNGUKA
Baada ya kupimwa na kupatiwa dawa za kutumia, baba Diamond aliliambia
gazeti hili kuwa, anamshukuru daktari huyo kwani ameweza kugundua tatizo
linalomsumbua na kwamba anaamini dawa alizopewa zitamsaidia.
“Kwa kweli ni Mungu tu, hali yangu ni mbaya, miguu inanisumbua kwa zaidi
ya miaka nane sasa. Inauma, imevimba na inabadilika rangi kuwa myeupe.
Inakuwa kama inatoka mabakamabaka. Kiuchumi siko vizuri kabisa.”
NGOZI IMEATHIRIKA
“Dk. Fadhili amenipima, amebaini ngozi yangu imeathirika vibaya.
Amenitajia tatizo langu kitaalamu na amenipa dawa za kutumia, lakini pia
amenielekeza mazoezi maalum ambayo natakiwa kuyafanya,” alisema baba
Diamond huku uso wake ukijaa simanzi.
AMWAGA SHUKRANI
Baba Diamond alipoulizwa kama alimueleza mwanaye Diamond kuhusu suala
hilo wakati alipozidiwa, alisema hakuona na haoni sababu ya kumwambia
kwani analijua na hapendi kuendeleza malumbano na mwanaye lakini
anamshukuru Dk. Fadhili kwa kujitolea kumsaidia bila malipo yoyote.
“Sipendi kuendeleza malumbano, ninachokiangalia kwa sasa ni miguu yangu.
Nitamshukuru Mungu zaidi nitakapopona kabisa maana nimeshahangaika nayo
sana. Kipekee, kutoka moyoni nimshukuru Dk. Fadhili kwa kusikia kilio
changu na kunisaidia bure.
“Sikutegemea, mtu unaumwa, anakwambia anakutumia fedha ya teksi uende
hospitalini kwake akakutibu bure. Ni upendo wa hali ya juu na Mungu
amzidishie, pale alipotoa apabariki na apate zaidi,” alisema baba
Diamond.
DIAMOND ANASEMAJE?
Gazeti hili lilifanya jitihada za kutaka kumsikia Diamond anazungumziaje
suala hilo la ugonjwa hadi kufikia mzazi wake kusaidiwa na mtu baki,
simu yake haikuwa hewani lakini hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa
maandishi kupitia Mtandao wa WhatsApp ulioonesha ameusoma, bado hakujibu
chochote.
TUMEFIKAJE HAPA?
Baba Diamond amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo wa miguu ambapo awali,
mzazi huyo alisema anasumbuliwa na kansa ya ngozi lakini hata hivyo,
mwanaye Diamond amekuwa mzito kumsaidia kutokana na kile kinachodaiwa
kuwa ni mwanaume huyo kumtelekeza mama Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’
yeye akiwa mdogo.
MAJIBU YA DK. FADHILI
Juzi Jumatatu, Risasi Mchanganyiko lilimpigia simu daktari huyo na
kumuuliza kuhusu tatizo la baba Dimaond na namna alivyolishughulikia,
ambapo alijibu:
“Ha! Jamani, ugonjwa wa mtu ni siri kati yake na daktari, labda kama ataona sawa aseme yeye mwenyewe.”
Loading...
Chediel . Powered by Blogger.
Post a Comment