Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

WAZIRI AJIONEA MADUDU MTIHANI LA SABA


WATENDAJI wakuu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi jana walikuwa na kibarua kizito kuzungukia shule mbalimbali zenye wanafunzi wanaofanya mtihani wa Darasa la Saba nchini, huku Naibu Waziri Philipo Mulugo, akishuhudia madudu Dar es Salaam. Watendaji hao waligawana mikoa mbalimbali kufuatilia mwenendo wa mtihani huo wakiongozwa na Waziri Dk Shukuru Kawambwa ambaye alikuwa mkoani Pwani.

 Naibu Mulugo alikuwa Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine, alikumbana na matukio kadhaa ikiwamo kujionea wanafunzi wakianza mitihani saa tano badala ya saa 2:00 asubuhi. Shule alizoshuhudia Naibu Waziri huyo wanafunzi wakichelewa kuanza mitihani ni Ndumbwi iliyoko Mbezi Beach na Mbezi Juu ambazo wanafunzi wake walianza mtihani saa 5:30 asubuhi. Shule zote hizo zipo Wilaya ya Kinondoni. 

Ofisa Elimu wa Manispaa ya Kinondoni, Hassan Kalinga alimweleza Naibu Waziri huyo kwamba tatizo hilo lilitokana na kiongozi wa msafara kushindwa kutambua maeneo ya shule hizo. “Uzembe huu umesababishwa na jamaa mmoja anayeitwa Peter Jonas ambaye ndiye mkuu wa msafara. Amepotea njia badala yake ametumia muda mwingi akizunguka kutafuta shule wakati alitakiwa kutembelea maeneo hayo mapema,” alisema Kalinga. Baada ya maelezo hayo, Naibu Waziri Mulugo aliagiza mkuu huyo wa msafara achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za kazi. “Naomba utaratibu uendelee kama kawaida. 

Huyu jamaa atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria maana hatuwezi kuvumilia vitendo vya uzembe ambao unatokea makusudi na mwaka huu tumewapa taarifa mapema, kuweni makini na mitihani,” alisema Mulugo. Mbali na kasoro hiyo ya Dar es Salaam, mitihani hiyo pia imeripotiwa kuchelewa kuanza katika baadhi ya shule katika Wilaya za Kilombero na Kilosa mkoani Morogoro. 

Katika majumuisho yake baada ya kutembelea shule 12 Dar es Salaam, Naibu Waziri Mulugo alisema kuwa pamoja na kasoro hizo, hakuna kasoro kubwa nyingine. Alisema hadi jana mchana alikuwa hajapokea taarifa zozote za kuvuja kwa mtihani na kwamba watendaji wa wizara  walipeana jukumu la kutembelea shule mbalimbali kujionea wenyewe kinachoendelea. “Kwa kweli mwaka huu tumejipanga tofauti na miaka iliyopita lazima mtihani uheshimiwe na tunaamini vitendo vya wizi havitakuwapo,” alisema Mulugo. Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na waandishi wetu baada ya kumalizika kwa Somo la Sayansi walisema mtihani huo haukuwa mgumu.

“Mtihani siyo mbaya, kwa neema ya Mungu mambo yatakuwa mazuri,” alisema mmoja wa watahiniwa katika Shule ya Msingi Mivinjeni. Walalamikia mfumo mpya 

Baadhi ya wanafunzi wamelalamikia kitendo cha kupigia mistari majibu ya Somo la Hisabati jambo ambalo walidai kuwa linaweza kuwafelisha.  Wakizungumzia mtihani huo, baadhi ya watahiniwa wa Shule ya Msingi Mchikichini walisema walishangaa kuambiwa kuwa kila jibu la somo la hisabati linatakiwa kupigiwa mstari katikati ya herufi na endapo mstari ukizidi, mtahiniwa huyo atakuwa hatarini kufeli. “Maswali yaliyotoka ni ya kuchagua A,B,C. 

Ni tofauti na mwaka jana wenzetu walikuwa wanajaza jibu kama A au B lakini mwaka huu tunapigia mistari majibu, mstari ukizidi hata kama umepatia unakoseshwa. Baadhi ya watahiniwa wa Shule ya Msingi Rutihinda, Ilala walisema Mtihani wa Hisabati siyo mgumu isipokuwa watahiniwa hao wanaweza wakafeli kutokana na mfumo  mpya unaotumiwa sasa na Serikali. “Hatuuelewi huu mfumo, hatujafundishwa na kuelekezwa,  tunakutana nao kwenye mtihani jambo ambalo litatusababishia wanafunzi wengi kufeli,” alisema mmoja wa watahiniwa hao bila kutaja jina lake. 

Mmoja wa walimu wa Shule ya Msingi Nyeburu ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema mfumo huo utawaathiri watahiniwa na kwamba walitakiwa kupewa semina ya miezi mitatu kabla ya kufanya mtihani huo. “Unajua Watanzania bado tupo nyuma na huu mfumo wanaotumia ni kwa ajili ya kusahihisha kwenye kompyuta hivyo mwanafunzi akikosea kwa kuzidisha mstari jibu zima atakuwa amekosa,” alisema.
Chanzo:Mwananchi.
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top