• Kima cha chini sasa 200,000/-
WAKATI Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Celina Kombani, amekataa kutaja nyongeza ya mishahara ya kima cha
chini kwa madai kuwa ni siri, imebainika kuwa mishahara hiyo imeongezeka
kwa sh 30,000 tu.
Nyongeza hiyo inafanya kima cha chini cha mishahara ya watumishi wa
umma, kufikia sh 200,000 kutoka sh 170,000 za mwaka wa fedha uliopita
2012/2013.
Baadhi ya wabunge walio kwenye Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na
Utawala iliyokuwa ikijadili kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, waliliambia gazeti hili kuwa kima cha chini cha
mshahara kimeongezeka kwa sh 30,000.
Hata hivyo, wakati akifanya majumuisho ya wizara yake jana, Waziri
Kombani licha ya baadhi ya wabunge kumtaka atangaze kiwango
kilichoongozeka, alisema kuwa hawezi kufanya hivyo kwani mshahara wa mtu
ni siri.
“Kuhusu masilahi ya watumishi wa umma. “Hapa msinilazimishe kima cha
chini, hapana. Hata sisi wabunge tunapoona kwenye magazeti yakitangaza
mishahara yetu, hatufurahi kwa sababu mshahara ni siri yako,” alisema
Kombani.
Waziri alirejea kauli yake juzi wakati akiwasilisha mwelekeo wa bajeti
ya wizara yake kwamba kwa mwaka wa fedha 2013/2014 serikali imetenga
sh trilioni 4.7.
Kiasi hicho ni kwa ajili ya nyongeza ya mishahara na kugharamia
mishahara kwa watumishi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Wakala wa
Taasisi za Serikali.
Kwa mujibu wa Waziri Kombani, kiasi hiki cha sh trilioni 4.7, pia
kitatumika kugharamia ajira mpya 61,915, upandishwaji vyeo na nyongeza
za kawaida za mishahara za mwaka, pamoja na nyongeza za mishahara
kuanzia Juni 2013.
Mwaka wa fedha uliopita 2011/12, serikali ilitenga sh trilioni 3.7
ambapo mshahara wa kima cha chini uliongezeka kwa sh 20,000 na kufanya
kima cha chini kupanda kutoka sh 150,000 hadi sh 170,000.
Hata hivyo Waziri Kombani aliwataka watumishi kuwajibika kwani wapo
wanaolalamikia kutaka nyongeza ya mishahara, lakini hawataki kuwajibika.
Waziri Kombani alisema serikali imeandaa operesheni maalumu ya kufanya
uhakiki wa vyeti vya watumishi wote nchini ili kubaini walioingia
kazini kwa kutumia vyeti vya kughushi.
Alisema wapo baadhi ya waliotumia vyeti vya marehemu na wengine ndugu
zao ambao pia wameajiriwa katika majina mawili ya watu wanaofanana.
Wakati serikali ikiongeza mishahara kwa kiwango kidogo, Shirikisho la
Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), limekuwa likipendekeza kima cha chini
kiwe sh 300,000 na katika mwaka huu wa fedha, imependekeza kima cha
chini kiwe sh 400,000 ili kukabiliana na gharama za maisha
zilizoongezeka mara dufu.
NA TANZANIA DAIMA
Post a Comment