BAADA ya yaliyotokea wiki iliyopita katika shughuli ya uzinduzi wa
Bunge, watu wengi, hususan wanasiasa walio upande wa chama tawala, Chama
Cha Mapinduzi (CCM0, wameita kitendo cha wabunge wa vyama vya upinzani
kususia kusikiliza hotuba ya Rais Dk. John Magufuli ya uzinduzi wa Bunge
kuwa ni kitendo aibu.
Wabunge-wa-UKAWA-wakitoka-bungeni-Njonjo Mfaume
Uamuzi wa kugomea shughuli hiyo ulitokana na uwepo wa Rais wa Zanzibar,
Dk. Ali Mohammed Shein ambaye wapinzani wanadai hastahili kuendelea
kuongoza Zanzibar. Wapinzani walitaka rais wao halali, Seif Sharrif
Hamad, ndiye awepo.
Mmoja wa walioelezea fujo iliyotokea na kitendo cha mgomo wa wapinzani
kuwa ni cha aibu ni Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai, huku Rais Magufuli
mwenyewe akiita kitendo hicho kuwa ni cha kitoto.
Mimi nakataa. Sioni kuwa kitendo kile cha wapinzani ni cha aibu wala cha
kitoto. Kuna vitendo vya aibu vimefanyika nchi hii ambavyo ndio hasa
vimetufedhehesha mbele ya wageni.
Kwa mfano, nchi imeingia katika aibu kwa vitendo vya hujuma dhidi ya
demokrasia ambavyo vimekuwa vikitokea kila mwaka wa uchaguzi kule
Zanzibar na kuingiza nchi katika migogoro ya kisiasa.
Kutokana na migogoro hii ya kisiasa ya Zanzibar watu wamekufa na wengine
kupata ulemavu katika 20 iliyoita. Tanzania imetoa wakimbizi wa kisiasa
kwenda Kenya na sehemu nyingine duniani. Jumuiya ya Kimataifa, hususan
Commonwealth imekuja kujaribu kutupatanisha wakati sisi ndio tegemeo la
majirani zetu la kupatanisha wanapogombana. Na haya ndio mambo ya aibu.
Kuanzia uchaguzi wa 1995 ambao ni wa kwanza kufanyika baada ya
kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 hadi huu wa mwaka 2015
hakujawahi kuwa na uchaguzi uliopita bila kuzalisha migogoro mikubwa
Zanzibar.
Uchaguzi wa mwaka 1995 ambao CCM ilitangazwa kuwa mshindi ulizaa mgogoro
baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kudai kuwa imeporwa ushindi na kugoma
kumtambua rais aliyetangazwa. Taarifa za waangalizi wengi wa kimataifa
zilieleza masikitiko yao kutokana na vitisho dhidi ya raia na
udanganyifu katika kuhesabu kura, jambo ambalo waliamini huenda
lilipelekea matokeo yaliyotangazwa kuwa sio sahihi. Baadhi ya nchi
wafadhili kama Norway na Sweden zilisimamisha misaada kwa Zanzibar
kutokana na kadhia ile na hii kwa mtazamo wangu ndio aibu.
Kutokana na mgogoro huo, Jumuiya ya Madola ilisimamia mazungumzo ya
upatanishi na hatimaye kufikiwa makubaliano yaliyosainiwa Aprili 29,
1999. Yalikuwa ni makubaliano mazuri ambayo yangetekelezwa huenda
migogoro isingejirudia tena. Moja kati ya vipengele vya makubalino kuwa
zichukuliwe hatua za kuhakikisha kuwa chaguzi za miaka ijayo ziwe wazi,
huru, za kuaminika na zisiwe na mizengwe.
Hata hivyo, uzuri wa makubaliano ni kitu kingine, na dhamira ya kisiasa
ya kutekeleza makubaliano hayo, hususan kwa upande wa watawala, ni jambo
jingine.
Ni wazi kuwa makubaliano yale ambayo yalilenga katika kujenga misingi ya
kuimarisha demokrasia, utawala bora na utengamano hayakutekelezwa kwani
mwaka 2000 kulitokea mgogoro mwingine ambao ulizalisha wakimbizi
waliokimbilia Shimoni, Mombasa huko Kenya. Na hii nayo ni aibu nyingine.
Pia, kufuatia uchaguzi wa mwaka 2000, mnamo Januari 27, 2001, watu 31
waliuwawa, 48, walipata vilema vya maisha na 243 walijeruhiwa, baada ya
polisi kutumia nguvu kuzuia maandamano ya kupinga matokeo ya au uchaguzi
Unguja na Pemba. Hii pia ni aibu iliyotufedhehesha kama taifa. Wengi wa
wahanga hao walitoka kisiwani Pemba.
Chanzo cha mgogoro wa uchaguzi wa mwaka 2000 ilikuwa ni kufutwa kwa
matokeo ya uchaguzi na kuamuliwa kurudiwa katika majimbo kadhaa ambapo
CUF haikukubaliana na uamuzi huo na kuamua kususia uchaguzi wa marudio.
Katika uchaguzi huo wa marudio, CCM walijishindia kirahisi.
Mgogoro ukaendelea tena hata katika uchaguzi wa 2005, ambapo kwa mara
nyingine tena, CUF waligoma kuitambua serikali ya Rais Amani Abeid
Karume. Kutokana na kutoridhika kwa uwepo wa hali hiyo ya migogoro
iliyogawanya jamii ya Wazanzibar, baadhi ya wanasiasa kutoka CUF na CCM
walifanya jitihada ya kuanzisha mazungumzo ya kutafuta muafaka ambayo
ndio yaliyozaa mpango wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010 ambayo
ilikubaliwa na Wazanzibar wengi.
Mazungumzo yaliyozaa muafaka na ambayo yalifanywa na Wazanzibar wenyewe
yalianza Machi 2009 na kufikia tamati Novemba 2009 kwa mkutano wa Rais
Karume na Maalim Seif Sharif Hamad na kukubaliana kufuta tofauti za
kisiasa zilizoigawa jamii ya Wazanzibari kwa zaidi ya miaka 15. Labda ni
kutokana na muafaka wa kisiasa uliofikiwa uchaguzi wa mwaka 2010
haukuhijiwa sana, ingawa bado kulikuwa na figisu figisu nyingi.
Hata hivyo, mwaka 2015 umekuwa ndio kilele cha migogoro yote baada ya
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,
kuamua peke yake kufuta matokeo ya uchaguzi wote, ingawa Tume ya
Uchaguzi ya Tanzania, (NEC) haikufanya hivyo kwa matokeo ya Zanzibar.
Inasemekana Jecha alitangaza uamuzi ule wa kufuta matokeo kwa
kushinikizwa.
Jambo la kuzingatia ni kuwa kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa
Zanzibar mwaka huu waangalizi wote wameuita huru na wa haki, huku CCM
wakilalamika kuibiwa. Kitendo cha CCM kimetajwa kuwa ni sawa kutia mpira
kwapani katika mechi ya soka, baada ya kuona unaelekea kushindwa!
Nikimjibu Magufuli, walichofanya CCM Zanzibar si sahihi.
Kuna hoja nyingi za kitaalamu zinazotolewa kuhalalisha yaliyofanyika
Zanzibar, lakini yote hayo ni katika jitihada za kuficha aibu kubwa
kabisa kuliko zote. Aibu kubwa kuliko zote ni kuwa kuna maana mpya ya
demokrasia imetoholewa kule Zanzibar. Demokrasia Zanzibar maana yake ni
ushindi kwa CCM, na si vinginevyo.
Najua kuna sababu za baadhi ya Wazanzibar na hata wanasiasa wa Tanzania
Bara kuamua kutumia maana hii mpya ya demokrasia iliyotoholewa. Kule
Zanzibar, CCM wanasema walipindua na hivyo basi hawako tayari kutoa
serikali kwa vipande vya karatasi. Pia wanasema wana wasiwasi CUF
watarudisha Waarabu. Huku Bara tunaogopa Uislamu wa siasa kali, kama
ambavyo video maarufu ya William Lukuvi akizungumza kanisani
ilivyotudhihirishia.
Mimi sio mtaalamu wa yote mawili. Sijui undani wa siasa za kimatabaka za
Uarabu dhidi ya Weusi, Zanzibar. Kadhalika pia sijui ajenda halisi za
CUF na uhusiano wake na siasa kali za Kiislamu, ingawa nimewahi kusoma
makala ya Abdulrahman Kinana katika jarida moja huko nje akigusa suala
la ugaidi.
Hata hivyo, kwamba hatusemi yaliyo vifuani mwetu kwa uwazi na badala
yake tunatekeleza demokrasia ya hila na ghilba ni aibu kubwa. Tunamhofia
nani kusema na kutenda kile tunachoamini? Nashauri CCM waifute CUF
Zanzibar ili watawale peke yao badala ya kuendelea kuulea uhizbu na
siasa kali za CUF kisa wanataka kuonekana na wao ni waumini wa
demokrasia. Mimi sielewi kwa nini tunashindana katika uchaguzi kama
kushindwa si matokeo ambayo tutakubali hata siku moja?
Baada ya hayo niseme kuwa kitendo cha wapinzani kususia bunge sio cha
aibu. Ni kitendo kizuri cha kishujaa kuiambia dunia kuwa mambo si shwari
Zanzibar. Nitamshangaa balozi wa nchi ya kigeni ambaye atashangaa
kitendo kile kwa kiasi cha mshangao chini ya alioupata kwa yaliyotokea
Zanzibar. Sana sana wengi watatupa uzoefu wa vituko vikubwa zaidi
vilivyowahi kutokea katika mabunge ya nchi zao.
CHANZO: RAIA MWEMA
Post a Comment